Kamishna wa Idara ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk. John Mboya akitoa mafunzo kwa wahariri kuhusu dhana ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi walioshiriki semina ya Wahariri wa Vyombo vya Habari, jijini Arusha.
NA JOSEPHINE MAJURA, WFM Arusha
WAHARIRI
wa vyombo vya habari wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali
kutangaza miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini ili wananchi wafahamu
kazi kubwa inayofanywa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Ahadi
hiyo wameitoa jijini Arusha wakati wa kufunga semina ya wahariri hao
iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini lengo likiwa kuwajengea uwezo wahariri kuhusu
dhana ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Mhariri
wa Gazeti la Tanzanite Selina Mathew, Clouds Media Joyce Shebe,
Habarileo Bakari Kingoba, wameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa
kuandaa mafunzo hayo kwa wahariri kwani yamewajengea uwezo mkubwa
kuelewa dhana ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ambayo
bado ni changamoto kwa baadhi ya waandishi katika kuiripoti.
“Wataalamu
wametupa shule ya kutosha mambo mengi tulikuwa hatuyafahamu lakini
kupitia semina hii ya siku mbili tumejifunza mengi kwa kweli
tunaipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa mada ambazo zimekuwa
na tija kwetu na zimetoa mwelekeo wa nini kinafanyika kwenye dhana ya
Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi,” alisema.
Waliahidi
kwenda kuandika makala za kutosha ili kuelimisha jamii kuhusu dhana ya
PPP na namna itakavyoleta matokeo chanya kwa nchi kupitia uwekezaji
unaofanywa na Sekta Binafsi katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Aidha
Wahariri hao walishauri serikali isichoke kutoa elimu na kutangaza
miradi inayotekelezwa na serikali na kuongeza kuwa wao kama chombo cha
kutoa taarifa kwa umma wataendelea kutoa taarifa mbalimbali kuhusu
mafanikio ya serikali ili dhana potofu ya kuwa serikali haitekelezi
miradi kwa wakati iweze kufutika.
Kwa
upande wake, Janeth Mushi aliwapongeza wataalamu kutoka Idara ya Ubia
baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kwa mada mbalimbali
walizofundisha ikiwemo Dhana ya PPP, Sheria na Kanuni zake.
“Sisi
ni chombo cha kutoa taarifa kwa umma ni wakati sasa kwa taasisi na
wizara nyingne kuiga mfano huu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wa
kutujengea uwezo ili tuwe na uelewa mpana wa shughuli mbalimbali
zinazofanywa na serikali ili tuweze kuzitangaza na wananchi wajue kazi
nzuri na kubwa inayofanywa na serikali”, alisisitiza Bi. Mushi.
Naye
Mhariri wa Gazeti la Majira, Ruben Kagaruki alitoa ushauri kwa Wizara
ya Fedha na Mipango iandae mafunzo kwa ajili ya waandishi wa habari
kwa kuwa wao ndio wanaenda kuchukua taarifa hivyo ni vizuri nao pia
wakapatiwa mafunzo ya masuala ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta
Binafsi ili wawe na uelewa mpana katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa
upande wake, Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema, John Daniel, aliishauri
serikali kupitia Wizara hiyo kusimamia kwa hali na mali utekelezaji wa
Sheria na Kanuni za PPP, bila kuruhusu mianya ya rushwa na kupewa watu
ambao hawana uwezo wa kutekeleza miradi hiyo na kusababisha
ucheleweshwaji na miradi kutokamilika kwa wakati.
Daniel
aliongeza kuwa ni vyema Wizara ya Fedha na Mipango ikaongeza muda
wakati mwingine wakiandaa semina ili kutoa nafasi kwao kujifunza mambo
mengi kwa weledi zaidi kwa kuwa elimu waliyoipata ni sehemu tu katika
dhana nzima ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Wizara
ya Fedha na Mipango kupitia Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kimekuwa
na utaratibu wa kufanya semina na wahariri wa vyombo vya habari nchini
lengo likiwa ni kuwajengea uwezo wa kutoa taarifa za wizara hiyo kwa
usahihi.
Hadi
sasa wizara imeshafanya semina kwa wahariri wakitokea kwenye vyombo vya
habari zaidi ya 40 katika nyanja mbalimbali kuhusu majukumu
yanayotekelezwa na wizara ikiwemo masuala ya Huduma Ndogo za Fedha,
Mfumo wa Kielektroniki wa Malipo ya Serikali (GePG) na semina hii ya
masuala ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.
Kabla
ya kufunga semina hiyo, Kamishna wa Idara ya Ubia kati ya Sekta ya Umma
na Sekta Binafsi Dkt. John Mboya, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, aliwakabidhi Wahariri vyeti vya kushiriki semina hiyo
kwa ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment