HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 14, 2021

Benki ya CRDB yashinda Tuzo ya Benki bora Tanzania ya Global Finance kwa mara ya tatu mfululizo

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akifurahia tuzo ambazo Benki hiyo imezipata ya “Benki Bora Tanzania” na “Benki inayoongoza kwa Ubunifu” ilizotunikiwa na jarida la Global Finance. Waliobeba tuzo hizo ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa (kushoto) na Meneja Mipango ya Biashara, Masele Msita. (Na Mpiga Picha Wetu).


Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutambulisha tuzo ambazo Benki hiyo imezipata ya “Benki Bora Tanzania” na “Benki inayoongoza kwa Ubunifu” ilizotunikiwa na jarida la Global Finance.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akifurahia tuzo ambazo Benki hiyo imezipata ya “Benki Bora Tanzania” na “Benki inayoongoza kwa Ubunifu” ilizotunikiwa na jarida la Global Finance.

 

 Dar es Salaam, Tanzania

Benki ya CRDB imewashukuru wateja na wadau wake kwa kuchaguliwa kuwa Benki bora nchini Tanzania kwa mara ya tatu mfululizo na jarida la kimataifa la Global Finance huku pia ikitajwa kuwa Benki inayoongoza kwa ubunifu. Benki ya CRDB imekuwa miongoni mwa benki 35 Afrika zilizotajwa kuwa bora na jarida hilo mashuhuri la nchini Marekani.

Akizungumza katika mkutano na Waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu ya benki hiyo mtaa wa Azikiwe, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela aliwahukuru wateja na wadau wa benki hiyo kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa mageuzi ya biashara (business transformation) ambao kwa kiasi kikubwa umesaidia kupata tuzo hiyo.

“Tunajivunia kupata tuzo hii kwa mwaka watatu mfululizo. Niwashukuru wateja, wanahisa na washirika wetu wa biashara kwa kuendelea kutuamini na kutufanya kuwa bora zaidi. Hii sio tuzo ya Benki ya CRDB peke yake, ni tuzo ya Watanzania wote,” alisema Nsekela.

Nsekela akibainisha mafanikio hayo pia yamechangiwa na kuimarika kwa biashara ya benki hiyo na ushiriki wake katika kuimarisha uchumi katika kipindi ambacho Taifa na dunia inapambana na changamoto za virusi vya corona (COVID-19). Kuimarisha biashara Benki ya CRDB mwaka jana ilitoa unafuu kwa wateja wake katika sekta zilizoathiriwa zaidi na corona.

“Hii ilisaidia wafanyabiashara na wajasiriamali wengi ambao ni wateja wetu kupanga mikakati mbadala iliyopelekea kufanya vizuri katika soko. Hii inadhirika katika matokeo ya kifedha kwani mikopo chechefu ilipungua hadi kufikia asilimia 4.4 kulinganisha na asilimia 5.5 mwaka 2019,” aliongezea Nsekela. Pamoja na changamoto za corona, Benki ya CRDB mwaka 2020 ilipata faida baada ya kodi ya shilingi bilioni 165.2 ikiwa ni ongezeko la asilimia 37.5.

Benki hiyo pia ilishirikiana kwa ukaribu na Serikali kuhakikisha vifaa kinga na tiba vinapatikana katika hospitali na vituo vya afya kote nchini kwa kuchangia katika mfuko wa maafa uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Katika upande wa elimu, Benki ya CRDB ilishirikiana na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kuendesha kampeni ya namna ya kujikinga na virusi hivyo vya corona.

“Benki yetu pia iliendesha kampeni maalum ya kuhamasisha wateja na Watanzania kutumia huduma za kidijitali ‘Popote Inatiki’ kupata huduma na kuachana na matumizi ya pesa taslimu kama ilivyoshauriwa na wataalamu wa afya,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka jana miamala ya wateja iliyofanyika katika mifumo ya kidijitali ikiwamo huduma ya SimBanking ilifikia asilimia 89.

Aidha aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara nchini ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa na mchango katika kuimarika kwa biashara nyingi ikiwamo sekta ya fedha. Nsekela alisema benki hiyo imeendelea kuunga mkono serikali katika jitihada zake za kuimarisha uchumi hususani katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Maradi wa Umeme wa Maji wa Nyerere (Stieglers).

Akizungumzia kuhusu tuzo ya ubunifu ambayo benki hiyo imetunikiwa, Nsekela alisema inatokana na huduma ya SimBanking mpya ambayo inawezesha wateja kufungua akaunti wenyewe (Self-Account Opening). Huduma hiyo imetambuliwa kama ubunifu wenye mchango mkubwa zaidi katika kuchochea ujumuishi wa kifedha nchini ‘financial inclusion.’

"Teknolojia na ubunifu vimeiwezesha benki yetu kutoa huduma bora kwa haraka, urahisi na kufikia watu wengi zaidi pale walipo," alisema.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Benki ya CRDB alisisitiza kuwa benki yake itaendelea kutilia mkazo katika kufikisha huduma kwa Watanzania wengi zaidi na kubuni huduma bunifu zinazokidhi mahitaji ya makundi mbalimbali ya wateja na sekta mbambali za uchumi nchini.

Katika taarifa yake Mkurugenzi na Mhariri Mkuu wa Jarida la Global Finance, Joseph Giarraputo, mchapishaji na mkurugenzi wa uhariri wa Global Finance alisema washindi tuzo za mwaka 2021 ni zile benki ambazo zilijikita katika kuwawezesha wateja kuvuka changamoto zilizosababishwa na corona na kuimarisha uchumi. Aidha alisema Jarida hilo pia limetazama matokeo ya kifedha kwa mwaka 2020.
 
"Benki ya CRDB imekuwa na mchango mkubwa kwa wateja na uchumi mwaka 2020. Ama hakika ilidhihirisha kuwa ni benki kiongozi kwa namna ambavyo ilikidhi mahitaji ya wateja na jamii kwa katikati ya changamoto. Pamoja na kujitoa kwao, wameweza tumeshuhudia ukuaji mkubwa katika biashara yao" alisema Giarraputo.

Katika orodha kamili iliotolewa karibuni na Jarida la Global Finance, kundi la majaji lilifanya upembuzi kwa benki zilizopo kwenye nchi 150 duniani kote. Benki ya CRDB imetunukiwa kwa upande wa Tanzania, ikungana na benki nyengine tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda.

Jarida la Global Finance linachapishwa na GFMag.com mtandao wa kuaminika katika upembuzi wa mahesabu na uwekezaji la New York, nchini Marekani.


 

No comments:

Post a Comment

Pages