HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 17, 2021

DKT. CHAMURIHO AFANYA MAZUNGUMZO NA MWAKILISHI WA SHIRIKA LA WFP

 


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt Leonard Chamuriho (kushoto) akiwa kwenye mazungumzo na Mwakilishi shirika la chakula Duniani hapa nchini Bi.Sarah Gordon-Gibson, alipomtembelea Waziri Chamuriho ofisini kwake.

 

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mha. Dkt. Leonard Chamuriho, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), nchini Tanzania, Bi. Sarah Gordon – Gibson jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili uboreshaji wa usafiri wa  reli, anga na meli katika maziwa makuu.

Katika mazungumzo  hayo  Dkt. Chamuriho, amemweleza mwakilishi huyo kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imedhamiria  kuendelea kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji katika Maziwa Makuu, ikiwemo Ziwa Victoria na Tanganyika ambako WFP wanapitisha mizigo yao.

Aidha, amemueleza kuwa Serikali imeshasaini mikataba mitano ya ujenzi na ukarabati wa meli ambazo zitagharimu zaidi ya shilingi bilioni 438.

"Serikali imeshaingia makubaliano ya ujenzi na ukarabati wa meli hizo ambao utaanza hivi karibuni kwa ajili ya kutoa huduma katika katika Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria na Bahari ya Hindi, ikiwa ni jitihada za kuimarisha usafirishaji katika Ushoroba wa Kati", amefafanua Dkt. Chamuriho.

Kuhusu usafirishaji wa njia ya reli, Dkt. Chamuriho, amemueleza mwakilishi huyo kuwa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), sehemu ya Mwanza hadi Isaka umeshaanza na unatarajiwa kukamilika mwaka 2024, ambapo sehemu ya  Dar es Salaam hadi Morogoro ujenzi umefikia asilimia 92 na  Morogoro hadi Makutupora asilimia 65.

Ujenzi wa reli hiyo ukikamilika utasaidia kurahisisha usafirishaji wa abiria, bidhaa, mizigo na vyakula  na hivyo kukuza uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake Mwakilishi wa WFP, Bi. Sarah  Gordon - Gibson, amemhakishia Mhe. Waziri kuwa Shirika hilo litaendelea kutumia Bandari ya Dar es Salaam na Reli ya kati kusafirisha shehena za vyakula kupeleka katika nchi za Uganda, Sudan na DRC kwani kutumia Bandari ya Dar es Salaam ni nafuu ukilinganisha na Bandari nyingine.

No comments:

Post a Comment

Pages