TAMASHA la Majimaji Selebuka msimu wa saba linatarajiwa kurindima kuanzia Julai 24 hadi 31 mwaka huu mjini Songea, Ruvuma ambapo mwaka huu linatarajiwa kuja kivingine likiwa na mabadiliko makubwa.
Tamasha hilo linalofanyika kila mwaka huandaliwa na Taasisi ya Songea Mississippi Foundation (SOMI), ambapo mwaka huu watashirikiana na Mpingo Conservation and Development Initiative (MCD), kihakikisha msimu wa saba unafana na linakwenda na kaulimbiu ya 'Misitu Ni Uchumi'.
Kwa mujibu wa Mratibu wa tamasha hilo, Reinafrida Rwezaura, tamasha la mwaka huu litapambwa na matukio mbalimbali ikiwemo Michezo, Ngoma za asili, utalii wa ndani, maonyesho ya biashara, nyama choma na mdahalo kwa shule za sekondari.
Rwezaura, alisema katika Michezo kutakuwa na Riadha Mbio za uwanjani, soka kwa shule za sekondari na timu za kata, Mbio za Baiskeli, Sanaa ya uchoraji na Ngoma za asili.
Mratibu huyo, alifafanua kuwa Baiskeli wanaume watachuana Kilomita 100 huku wanawake wakionyeshana kazi Kilomita 25.
Alibainisha viingilio kwa upande wa washiriki wa Mbio za Baiskeli itakuwa ni Sh. 10,000 kwa washiriki kutoka ndani ya Mkoa wa Ruvuma huku wale wa nje ni Sh. 25,000.
Kwa upande wa maonyesho ya biashara, alisema mtu mmoja atalipa Sh. 30,000 Kikundi Cha Wajasiriamali saba ni Sh. 100,000 huku kwa kampuni ni Sh. 500,000.
"Kwa upande wa Utalii wa ndani tutakuwa na vionjo mbalimbali vya kuvutia ikiwemo Nyama Choma juu ya Milima ya Matogoro ambapo gharama itakuwa Sh. 30,000, nyama choma Ruhila Zoo Sh. 30,000, safari ya Mbamba Bay Beach Sh. 150,000 wakati kutalii Makumbusho ya Mashujaa wa Majimaji itakuwa Sh. 10,000," alisema Rwezaula.
Mratibu huyo, alitaja zawadi mbalimbali zitakazotolewa kuwa kwa upande wa soka shule za sekondari, bingwa ataondoka na Kombe, jezi jozi mbili na mipira miwili, mshindi wa pili atazawadiwa Kombe, jezi jozi moja na mpira mmoja huku wa tatu akijipoza na jezi jozi moja.
Kwa upande wa timu za Kata, Rwezaula alisema Bingwa atajipatia Kombe na kitita cha Sh. 700,000 huku wa pili akipata Sh. 500,000 na wa tatu Sh. 300,000.
Aliongeza kuwa, katika mdahalo shule itakayoshinda itapata Kikombe na cheti huku wanafunzi wawili watakaowakilisha wataondoka na 'tablet' kila mmoja, mshindi wa pili Kikombe, cheti huku wawakilishi wa pili wakipata mabegi kila mmoja na shule mshindi wa tatu itazawadiwa Kikombe na cheti.
Mratibu huyo, alibainisha kuwa katika kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Misitu ni Uchumi', wataendesha zoezi la kuandaa kitalu cha upandaji miti.
Alitoa wito kwa washiriki kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Ruvuma, kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo ili kitumia fursa mbalimbali zilizipo.
Mgeni rasmi katika tamasha hilo, anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Wilbert Ibegwe.


No comments:
Post a Comment