Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni.
NA PETER HAULE, WFM
NAIBU
Waziri wa Fedha na Mipango Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, ameiagiza
Benki ya TIB kuhakikisha madeni na fedha zote za mikopo zaidi ya Sh.
Bilioni 535.3 zilizokopeshwa kwa wateja wao bila kufuata taratibu pamoja
na wadaiwa sugu zinarejeshwa ili zitumike kutoa mikopo kwenye maeneo
mengine yenye tija.
Mhandisi Masauni ametoa maagizo hayo jijini
Dar es Salaam alipotembelea Benki hiyo na kufanya mazungumzo na
Menejimenti ya Benki hiyo na wafanyakazi, katika mwendelezo wa ziara
zake za kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo jijini Dar es
Salaam.
“Kwa njia yeyote ile ni lazima fedha za wananchi
zirejeshwe hivyo nawaagiza pia kuleta mapendekezo Serikalini ili
kuangalia iwapo kuna eneo ambalo Serikali inaweza kuingilia kati
kuhakikisha tunaokoa fedha za wananchi zilizowekezwa katika miradi isiyo
na tija”, alieleza.
Mhandisi Masauni alisema kuwa nchi
inapoelekea inahitaji kuona Benki hiyo inashiriki kikamilifu katika
ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati ya Taifa kwa kuiwezesha Serikali
kukopa katika taasisi za fedha za ndani badala ya kukopa kutoka benki za
nje na kuwataka watendaji wa benki hiyo kusimamia ipasavyo Benki ili
jambo hilo liwezekane.
Aidha Mhandisi Masauni ameitaka Benki hiyo
ihakikishe mikopo yote inayotolewa iwe na tija ili kuepuka mikopo
chechefu na kufadhili miradi inayoweza kuisababishia hasara Benki hiyo
na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya
Wakurugenzi ya Benki ya TIB, Mary Mashingo, alisema, kuwa taasisi hiyo
inashauku ya kushiriki katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati
inayoendelea nchini na kusaidia katika kutekeleza Sera katika sekta
mbalimbali za maendeleo hivyo itashirikiana na Serikali kubuni mbinu za
kuzirejesha fedha zilizokopeshwa kabla ya mwaka 2016 na pia kupunguza
riba kwa kuwatumia wataalam mbalimbali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji
wa Benki ya TIB, Charles Singili, alisema kuwa Benki yake kwa
kushirikiana na Wataalam kutoka Wizara hiyo wanafanya jitihada ya
kuhakikisha fedha hizo, zikiwemo Sh.Bilioni 168 ambazo kesi zake ziko
mahakamani na kiasi kingine cha Sh. Bilioni 368 zilizoko mikononi mwa
wadaiwa sugu zinarejeshwa ili zitumike kutoa mikopo kwa wawekezaji
wengine ili kuchochea upatikanaji wa ajira na pia kodi ya Serikali
kupitia miradi hiyo.
Vilevile alieleza kuwa namna pekee
itakayoongeza wigo wa kodi ni uwepo wa miradi mingi inayozalisha, na
kumhakikishia Masauni kwamba Benki yake itazifuatilia fedha hizo ili
ziboreshe mizania ya mtaji ya Benki hiyo na kuziwekeza katika meneo
yatakayosaidia kujibu matatizo ambayo nchi inakabiliana nayo na
kuboresha maisha ya wananchi.
No comments:
Post a Comment