Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR Mageuzi, Martha Chiomba akizungumza na wanawake Wanachama cha wa chama hicho katika Ukumbi wa Fimbo wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Na Selemani Msuya
KATIBU Mkuu wa Chama cha NCCR, Mageuzi, Martha Chiomba, amewataka Wanzania kuweka muafaka wa kitaifa na kuunganisha nguvu kabla ya kuenda kudai Katiba mpya.
Chiomba aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya mafunzo kwa wanawake wa chama hicho kutoka Mbagala wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Alisema popote duniani palipotokea muafaka wa kitaifa kulisaidia jamii husika kuwa pamoja na kupata Katiba sahihi ambayo inatokana na wananchi.
“Niwaombe wakina mama wenzangu tuungane katika kipindi hiki kwa kuwa na muafaka wa kitaifa ambao utatuwezesha kupata Katiba inayotokana na sisi,” alisema.
Katibu huyo alisema wanawake ni jeshi kubwa hivyo likiungana na kushirikiana linaweza kutoka na matunda mazuri ambayo yanaweza kuchochea maendeleo.
Alitolea mfano Katiba ya Zanzibar ambayo imeweza kuchangia upatikana wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo inashirikisha vyama vyote kulingana na kura ambazo vyama vimepata.
Chiomba alisema iwapo Watanzania wataunganisha nguvu hakuna jambo lisilowezekana hivyo kuasisitiza mshikamano kama chachu ya kufikia malengo.
Alisema Katiba ya sasa imeonesha mapengo mengi hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya Watanzania ambao wanaendelea kuwa masikini.
Aidha, Chiomba aliwataka wanawake hao wasibweteke na kidogo walicho nacho bali wajitume na kufanya kazi halali ili kuongeza kipato cha kusaidia maisha yao na familia zao.
“Ipo dhana ya kuwa sisi ni watu tegemezi sio kweli tunapaswa kufanya kazi kwa nguvu zote kwa kuwa hali hiyo itatochochea sisi kujiamini, kuthubutu na kuheshimika kwenye jamii. Mimi ni mwanamke ambaye najiamni kwa sababu nipo vizuri kiuchumi na kielimu, tusibaki nyuma kila fursa tuikimbilie,” alisema.
No comments:
Post a Comment