Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akizungumza na Vyombo vya Habari kuhusu masuala mbalimbali ya tozo za miamala ya simu leo Jijini Dar es Salaam kulia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile.
NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba , amesema Serikali
imesikia kilio na maoni ya wananchi kuhusu tozo mpya ya miamala ya simu
na kuwaomba wawe watulivu wakati jambo hilo linatafutiwa ufumbuzi.
Dk Nchemba ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na
vyombo vya habari huku akiwa ameambatana na Waziri wa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano Dk Faustine Ndugulile.
“Kuna maaneo ambayo wananchi wametoa ushauri na kuelezea namna ambavyo
jambo hili linawagusa lakini pia tumepokea maoni ya maeneo yanayotakiwa
kutoa elimu zaidi ili kujenga uelewa wa pamoja ikiwa ni pamoja na
viwango vinavyokatwa kwa anayetuma na anayetoa lakini pia kuhusu mantiki
ya jambo lenyewe,” alisema.
Alisema kuwa jambo la tozo za miamala linatekelezwa kupitia Sheria
iliyopitishwa na Bunge lakini kuna Kanuni za utekelezaji zinazo mhusu
yeye kama Waziri wa Fedha na Mipango na maeneo mengine yanahusu Wizara
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambazo zitajadiliwa na kupatiwa
ufumbuzi.
Dk. Nchemba alisema, kuwa leo atakuwa na kikao kilichoitishwa na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, kujadili suala hilo na pia kutakuwa na kikao
kingine cha Mawaziri wa Wizara zote watakaojadili na kuchambua kwa kina
suala hilo.
“Lakini Tayari Rais Samia Suluhu Hassan naye alishaguswa na jambo hili,
amesikia maoni ya watanzania wote na yeye ametoa maelekezo kwamba
tuyafanyie kazi maoni hayo,
…Nitoe rai kwa wananchi kuwa watulivu kwenye jambo hili, tutaendelea
kuelezea na kutoa ufafanuzi kwenye kila maeneo yanayohitaji ufafanuzi na
tutachukua hatua kwenye maeneo wanayohitaji kuchukuliwa hatua ili
ujenzi wa taifa letu uendelee kama ambavyo wananchi wamekuwa na shauku
kubwa kuona ujenzi wa Taifa letu unaendelea kwa ajili ya maendeleo ya
nchi,” Aliongeza.
Dkt. Nchemba aliwaonya watu wenye nia mbaya ambao mara zote wanapenda
kupotosha ama kubadili dhana au maana halisi ya jambo lilivyokusudiwa na
kuwataka wasifanye hivyo, kwani mambo haya yana maslahi mapana kwa
nchi.
“Haya ni mambo ya kisheria, Sheria za nchi zinatakiwa kuheshimiwa, ni mambo ambayo ni ya kikanuni yanayohitaji uelimishaji.
…Tutaendelea kufafanua lakini yale yanayotakiwa kufanyiwa kazi niwaahidi
watanzania, tutaendelea kuyafanyiakazi kama ambavyo viongozi wetu wakuu
wamesema” Alisisitiza.
Alisema tayari aliwapa maelekezo wataalam wa mifumo kuangalia vipengele
vya Sheria ya Mifumo ya malipo Serikalini pamoja na Sheria ya
Mawasiliano ya Mtandao (EPOCA) inayoelezea kuhusu masuala ya miamala kwa
njia ya mtandao na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kufikia muafaka
wa jambo hilo.
Alitoa rai kwa watanzania waendelee kumuunga mkono Rais Samia Suluhu
Hassan katika Dira yake ya kuhakikisha anasukuma mbele shughuli za
maendeleo ya nchi na ili tuwakomboa na kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Kwa upande wake Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Dk.
Faustine Ndugulile alibainisha kuwa Wizara yake pia ambayo inaguswa moja
kwa moja na tozo hizo imeendelea kupokea maoni na kuchakata taarifa
mbalimbali tangu tozo hiyo ianzishwe na kumwahidi Waziri wa Fedha na
Mipango kwamba atampa ushirikiano kuhakikisha kwamba maelekezo
yaliyotolewa na viongozi yanatekelezwa.
Alirejea kutoa wito kwa watanzania kuwa watulivu wakati jambo hilo
linafanyiwa kazi na kusema kuwa Serikali ni sikivu na itafikia muafaka
mzuri.



No comments:
Post a Comment