HABARI MSETO (HEADER)


July 10, 2021

UCSAF kutumia shilingi bilioni 32 kupeleka mawasiliano



Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba, akimpatia vitabu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile alipotembelea banda la mfuko huo kwenye maonesho ya 45 ya DITF.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk. Faustine Ndugulile, akizungumza na waandishi wa  alipotembelea banda la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)huo kwenye maonesho ya biashara ya kimataifa.

 

Na Selemani Msuya

MFUKO wa Mawasiliano  kwa Wote (UCSAF), unatarajia kutumia shilingi bilioni 32 katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano pembezoni mwa Tanzania na mashuleni.

Hayo yamesemwa na Mtendaji UCSAF Justina Mashiba wakati akizungumza na gazeti hili kwenye kwenye Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba yenye kauli mbiu ' Uchumu kwa Ajira na Biashara Endelevu'  yanayofanyika katika Viwanja vya Julius Nyerere Temeke jijini Dar es Salaam.

Mashiba alisema UCSAF imejipanga katika kuhakikisha huduma za mawasiliano na mtandao zinafikia Watanzania wote kwa miaka mitano ijayo hivyo wanaendelea kuwezesha wadau ili kufikia lengo hilo.

Alisema kiasi hicho cha shilingi bilioni 32 zitatekeleza miradi mbalimbali hasa vijijini na mipakani ambapo huduma ya mawasiliano ina changamoto.

“Jukumu la kupeleka huduma ya mawasiliano tunalitekeleza kwa kushirikiana na kampuni zilizopewa lesini na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kuhakikisha watu wa kijijini kama Narung’ombe na mipakani kunapata utatuzi wa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo na uchumi wa nchi,” alisema.

Alisema hii ni mara ya pili wao kushiriki Maonesho ya Sabasaba ambapo wametembelewa na wageni zaidi ya 500 lakini ageni 63 wameelezea changamoto ya mawasiliano hasa vijijini hivyo kupitia changamoto hizo watahakikisha huduma za mawasiliano zinapatikana.

Mashiba alisema pia watahakikisha wanatatua changamoto ya maeneo ya mipakani kusikiliza redio za nje ambapo watawezesha vyombo vya habari kuwa na uwezo wa kufika huko.

Aidha, alisema wanatarajia kutoa komputa 800 kwa shule ambapo kila shule itapatiwa komputa tano na mashine ya kuprinti moja lengo likiwa ni kurahisisha huduma za TEHAMA kwa walimu na shule.

Mkurugenzi huyo alisema UCSAF ipo tayari kuwezesha kada zote ambazo zinachangia upatikaji wa huduma ya mawasiliano kupatikana kwa urahisi.

Akizungumzia mipango hiyo ya UCSAF Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile alisema changamoto hizo za mwasiliano pembezoni na katika wilaya kumi ambazo bado zina changamoto zitataliwa mwaka huu wa fedha.

Ndugulile alisema kwa kuanzia UCSAF imewezesha usikivu wa redio ya TBC ambapo studio ya Dodoma na Arusha zimeboreshwa.

Alisema mikakati ya wizara yake kwa kushirikiana na UCSAF ni kuleta mapinduzi katika kada ya mawasiliano ili kuchangia ukuaji wa uchumi na maendeleo.
 

No comments:

Post a Comment

Pages