Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza kabla ya kusaini mikataba miwili iliyoingiwa kati ya Chuo hicho na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Kituo cha Mafunzo na uhusiano wa Kimataifa (MS TCDC) juzi jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa (Kulia) akibadilishana mikataba na Mkurugenzi wa mipango wa MS-TCDC Sara Ezra Teri (Kushoto) mara baada ya pande zote kusaini mikataba jijini Dar es Salaam juzi.
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga wakionyesha mikataba iliyoingiwa kati ya Chuo hicho na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) juzi jijini Dar es Salaam.
NA MWANDISHI WETU
CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeshauriwa kuendelea kuingia makubaliano na wadau wa sekta ya usafirishaji wa ndani na nje ya nchi ili kuweza kupata msaada mkubwa wa kuweza kuzalisha watalaamu wa kutosha na wabobezi ambao watakidhi mahitaji ya soko.
Akizungumza kabla ya kushuhudia mikataba miwili iliyoingiwa kati ya Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Kituo cha Mafunzo na Uhusiano wa Kimataifa (MS TCDC) katika kuboresha usawa wa jinsia, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA), Hamza Johari alisema:
“Ni muhimu sana kuendelea kuingia katika makubaliano na wadau wa sekta hii ya usafirishaji ili tuweze kuzalisha wafanyakazi wa kutosha na walioiva ambao watakidhi mahitaji ya sekta hii ya usafirishaji.”
Johari, ambaye alikuwa mgeni rasmi aliongezea:
"Mikataba hii ambayo NIT inasaini na LHRC na MS-TCDC itaweza kuboresha kwa kiasi kikubwa eneo la jinsia na usawa katika mafunzo yanayotolewa chini ya Mradi wa EASTRIP ambao unatekelezwa na NIT."
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya NIT kwenye Kituo cha Umahiri cha Taaluma za Usafiri wa Anga na Opresheni za Usafirishaji alisisitiza:
"Nina hakika kwamba baada ya kusainiwa kwa makubaliano haya, mradi wa Benki ya Dunia uliotekelezwa na Chuo utaboreshwa sana haswa katika eneo la jinsia."
Johari ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirika la Huduma za Usafiri wa Anga (CANSO) kwa Afrika, aliongeza.
“Tunataka kuona Chuo Chetu cha NIT kinakuwa maahiri sana kwenye sekta ya usafirishaji, wiki iliyopita nilipokuwa kwenye mkutano mkuu wa Shirika la Huduma za Usafiri wa Anga (CANSO) ambapo mimi ni mwenyekiti wa Africa, maazimio yalikuwa ni kuwa na vituo vya umahiri katika sekta ya usafiri wa anga. Kwa bahati nzuri kwenye nchi yetu tayari tunacho katika Chuo chetu hapa NIT.”
Kwa Upande wake Mkuu wa Chuo cha NIT Mhandisi. Prof. Zacharia Mganilwa alisema:
"Tumeamua kuingia makubaliano na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kituo cha Mafunzo na uhusiano wa Kimataifa (MS TCDC) ili waweze kutusaidia katika eneo la jinsia kwenye mradi tunaoutekeleza wa EASTRIP unaodhaminiwa na Benki ya Dunia.”
Profesa Mganilwa aliongezea kuwa mashirika hayo mawili ya LHRC na MS-TCDC ni wabobezi katika eneo la jinsia hivyo kwa kiasi kikubwa wataweza kuisadia NIT kufikia malengo yaliyowekwa na mradi huo.
Prof Mganilwa alisema kuwa mara nyingi masomo ya uhandisi yamekuwa yakitawaliwa sana na jinsia ya kiume na kuiacha nyuma jinsia ya kike, hivyo kwa ushawishi wa mashirika hayo mawili, Chuo kinategemea mabadiliko makubwa katika kuleta usawa wa kijinsia katika eneo hilo.
“Tunatumahi kuwa taasisi hizi mbili zitatoa ushawishi mkubwa zaidi kwa wanafunzi wa kike kuchagua programu hizo ambazo zilikuwa zinasomwa na wanaume wengi zaidi ya wanawake,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema: "Tunaahidi kutekeleza majukumu yetu ambayo tumekubaliana ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo kwenye masuala ya jinsia wanafunzi pamoja na waalimu kama inavyotakiwa na mradi wa EASTRIP."
Naye Mkurugenzi wa mipango wa MS-TCDC Sara Ezra Teri alisema: "Shirika letu linatoa programu za masomo ambazo zinalenga kuimarisha uongozi bora, utawala katika maeneo ya maendeleo katika nchi za Afrika. Hivyo, kwa makubaliano haya, tunaahidi kutoa maarifa bora kwenye eneo la jinsia kwenye uendelezaji wa mitaala ili kuweza kuweza kuboresha usawa wa kijinsia. "
Pamoja na juhudi za kukuza usawa wa jinsia, Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji kimepanga kuanzisha Scholarship ya Ubora katika eneo la Usafirishaji (Transport Excellence Scholarships - TES) kwa Wanafunzi wa Kike wa Kitanzania kusoma mafunzo ya muda mfupi, stashahada (diploma) na shahada (bachelor degree) na Udhamini wa Shahada ya Uzamili utakaotolewa kwa watanzania na wanafunzi kutoka nje ya nchi. Scholarships hizi zitatolewa katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi 2023/2024.
No comments:
Post a Comment