HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 15, 2021

Zaidi ya Majangili 420 wakamatwa kwa mwaka 2019/2020

 

 

Waandishi wa habari wanawake kutoka mikoa mabalimbali wakiwa katika picha ya kumbukumbu walipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 

Na Jasmine Shamwepu, Iringa


Katika kuhakikisha ulinzi unaimarishwa hifadhi ya Ruaha mkoani Iringa ,mamlaka ya hifadhi  ya taifa ya Ruaha  mkoani Iringa  imefanikiwa kukamata zaidi ya majangili 420 katika kipindi cha mwaka 2019 -2020 hali iliyopelekea idadi ya majangili kupungua katika hifadhi hiyo.

Hayo yamesemwa  na afisa mhifadhi daraja la kwanza kitengo cha Ulinzi  katika hifadhi ya taifa ya Ruaha mkoani Iringa  Jackson Laizer  wakati akifanya mahojiano maalum na waandishi wa habari ambapo amesema  wamekuwa wakifanya doria mbalimbali zikiwemo doria za ndege,doria za magari,doria za boti ,na doria za miguu .

Ametaja makosa waliyokutwa nayo majangili ikiwemo kuwinda wanyama,kuchungia hifadhini na kuvua samaki na ulimaji wa mashamba ambapo mwaka 2020/2021 kuna majangili kuna majangili 298 ambapo vikosi vya doria hutumia mtandao wa GPS kufuatilia mienendo ya majangili.

Laizer amewataja wanyama ambao wamekuwa wakiwindwa kwa wingi na majangii ni swala,tandala pamoja na pundamilia huku akibainisha aina nyingine ya ujangili ni ujangili wa ukataji miti na wamekuwa wakishirikiana na wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kutoa taarifa na kufanikisha kupanga vikosi vya doria kwenda kukagua na kukamata hali ambayo imesababisha idadi ya majangilikupungua.

Mhifadhi kitengo cha Ikolojia katika hifadhi ya taifa ya Ruaha Halima Kiwango amesema katika kitengo cha ikolojia wanasimamia shughuli zote zinazohusiana na wanyama ikiwemo afya,mwingiliano na mazingira ambapo amesema katika hifadhi hiyo kuna upekee wa mwingiliano wa aina kuu mbili za uoto wa migunga kusini na miombo kaskazini pia kuwa na wanyama aina ya kipekee ambao wanapatikana Hifadhi ya Ruaha pekee tofauti na waliopo katika hifadhi zingine.

Aidha,Halima amesema majukumu yao ni kuhakikisha asili ya ikolojia inabaki palepale huku akibainisha changamoto zilizoweza kujitokeza ni pamoja na changamoto za kukauka mto Ruaha kipindi cha nyuma na juhudi mbalimbali zimefanyika katika kuhakikisha hali inarudi katika hali ya kawaida.

Afisa Afya msaidizi kitengo cha Afya Wanyama pori   hifadhi ya taifa ya Ruaha Andrea Mbwambo  amesema magonjwa wanayoshughulika zaidi ni magonjwa yatokayo kwa binadamu kwenda kwa wanyama na kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu  ikiwemo kimeta pamoja na visababishi vya binadamu ikiwemo ajali.

Pia ,amesema kipaumbele kikubwa zaidi ni kwa wanyama ambao wapo hatarini kupotea hivyo kitengo cha afya kimekuwa kikifanya uangalifu wa hali ya juu ili kuweza kuwalinda wanyama hao.

Afisa uhifadhi kitengo cha mawasiliano  na jamii hifadhi ya taifa ya Ruaha Emaculata Ngowi amesema katika hifadhi hiyo kitengo cha mawasiliano kilianza mwaka 1961 na wamefanikiwa kutoa elimu ya uhifadhi  na namna ya wananchi kujiongezea kipato katika wilaya tano za Mufindi,Iringa,Chunya,Mbarali,na Chamwino .


Hifadhi ya Ruaha ilianza mwaka 1910 na kufikia mwaka 1964 ilisajiliwa rasmi baada ya kuendelea kuboreshwa zaidi na mwaka 2008 eneo la kusini mwa hifadhi katika pori la hifadhi ya Usangu pamoja na baadhi ya vijiji yaliongezwa na kuimarishwa ulinzi na kuifanya hifadhi kuwa na ukubwa wa kilometa za eneo 20,226 na kuifanya hifadhi kuwa ya pili kwa ukubwa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Pages