HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 09, 2021

Benki ya KCB yafadhili vijana 200 kujifunza ufundi stadi Chuo cha VETA Dar es Salaam


Jumla ya vijana 200 jijini Dar es Salaam wanatarajia kunufaika na mafunzo maalum ya ufundi stadi kwenye sekta ya ujenzi kupitia programu ya 2jiajiri inayofadhiliwa na  Benki ya KCB Tanzania.

Akizungumza wakati wa utiaji saini makubaliano ya utekelezaji wa mpango huo kati ya Benki ya KCB Tanzania na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) tarehe 7 Oktoba, 2021, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Benki hiyo, Margaret Mhina, amesema lengo la programu hiyo ni kuwezesha vijana kujipatia ujuzi ili kuweza kujiajiri mara tu wanapohitimu.

“Tunalenga kumtoa kijana kwenye fikra za kuajiriwa na kumpeleka kwenye mawazo ya kujiajiri na kuajiri vijana wengine… Tunaamini kabisa kuwa VETA ni sehemu sahihi ya kuwezesha vijana kujiajiri kwa kupitia mafunzo wanayoyatoa,” Amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujulu, ameishukuru Benki ya KCB kwa kutoa sehemu ya faida yao kufadhili vijana kujipatia mafunzo ya ufundi stadi kupitia chuo cha VETA Dar es Salaam, na kuongeza kuwa anaamini mafunzo hayo yatawezesha vijana hao kujitegemea, kuboresha maisha yao na hatimaye kukuza uchumi wa nchi.

“Tunawapongeza sana KCB kutokana na ukweli kwamba wameamua kuwekeza sehemu sahihi ambayo italeta matokeo endelevu na kuongeza chachu ya ukuaji wa uchumi. Vijana watakaopata mafunzo haya hawatakuwa tegemezi tena," Amesema.

Dkt. Bujulu amesema VETA itahakikisha kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa ufanisi ili hatimaye vijana hao wapate ujuzi stahiki utakaowawezesha kulitumikia Taifa kwa umahiri.

Mkuu wa Chuo cha VETA Dar es Salaam, Joseph Mwanda, amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa miezi mitatu kuanzia mwezi Oktoba, 2021 hadi Januari, 2022 katika fani za Uashi (Masonry & Brick laying), Umeme wa Majumbani (Electrical Installation), Ufundi Bomba (Plumbing & Pipe Fitting), Ufundi wa Aluminiam (Aluminium Works) na Usanifu na Upakaji Rangi (Painting & Sign Writing).

No comments:

Post a Comment

Pages