HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 22, 2021

Dk. Gwajima kunogesha siku ya lishe Tabora


Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Dk. Germana Leyna.

 

Na Irene Mark
 

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima anatarajiwa kuongoza kilele cha kuhitimisha Maadhimisho ya Siku ya Lishe kitaifa, ambayo kwa hapa nchini yanafanyika mkoani Tabora katika viwanja vya Nanenane Ipuli.

Maadhimisho ya Siku ya Lishe nchini kwa Mwaka huu yameanza Oktoba 18 mkoani Tabora yakiambatana na shughuli za maonesho na utoaji elimu ya masuala ya afya na lishe katika viwanja vya Nanenane Ipuli na yatahitimishwa siku ya kesho Oktoba 23, 202.

Akizungumzia sababu za uwepo wa wiki hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Dkt. Germana Leyna anasema bila afya bora hakuna taifa imara na afya hiyo inaanzia kwenye ulaji sahihi.

“Katika elimu tunayotoa kwa wananchi tunawaambia mlo kamili ni ule wenye makundi yote matano ya vyakula kuwa kwenye sahani moja.

“Nani alisema spinachi, mchicha na kabichi tu ndio mboga za majani? Mnajua kwamba mchunga una madini mengi sana ni namna ya kuuandaa tu.

“...Tunachotakiwa kujua ni chakula gani kipo kwenye kundi gani la chakula, huwezi kula wali na ugali kwenye sahani moja maana hilo ni kundi la wanga, lazima sahani yako iwe na chakula kutoka kundi la wanga, protini, vitamini, nyama na tunda hapo tutasema ni mlo kamili,” alisema Dk. Leyna.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, mlo kamili unaondoa maradhi yatokanayo na uzito uliopitiliza na yasiyoambukizwa, mathalani shinikizo la damu, moyo, saratani, sukari, figo na mengineyo huku akisisitiza wananchi kufanya mazoezi.

“Maendeleo yamekuja na changamoto zake hasa uzito uliopitiliza unaosababisha viriba tumbo, watu hawatembei siku hizi na hawafanyi kazi za kutumia nguvu hasa mijini hili ni tatizo.

“Kwa kuwa hilo ni tatizo, kauli mbiu ya Siku ya Lishe  inasema ‘Lishe bora ni Kinga Thabiti Dhidi ya Magonjwa. Kula Mlo Kamili, Fanya Mazoezi, Kazi Iendelee’ tunahamasisha mazoezi na mlo kamili,” alisema Dk. Leyna.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk. Batilda Burian aliwahamasisha wakazi wa mkoa huo kutembelea maonesho mbalimbali ya vyakula yanayoendelea kwenye viwanja vya Nanenane Ipuli kwa lengo la kujifunza na kupata elimu ya Lishe bora.

“Maonesho haya yataongeza hamasa kwa wana Tabora na Watanzania kubadili utaratibu wa ulaji kwa kuzingatia mlo kamili wenye makundi yote matano kwenye sahani moja,” alisema Dk. Buriani.

Hii ni mara ya pili kwa Maadhimisho ya Siku ya Lishe nchini kufanyika tangu kuanzishwa kwake, ambapo kwa mara ya kwanza Siku ya Lishe Kitaifa ilifanyika Agosti 7,2020 mkoani Dodoma na kwa mwaka huu maadhimisho haya yanafanyika mkoani Tabora.

No comments:

Post a Comment

Pages