HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 22, 2021

DPP AONDOA MASHITAKA YA KUTAKATISHA FEDHA KESI YA MWANASHERIA WA IPTL

 Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI wa Mashtaka Nchini (DPP), amemuondolea mashitaka ya kutakatisha fedha aliyekuwa mwanasheria wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege.


Hatua hiyo imefikiwa jana baada ya upande wa Jamhuri kuomba kubadilisha hati ya mashtaka dhidi ya mshtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladslaus Komanya alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.


Hata hivyo, alidai kuwa  bado hawajafikia muafaka katika majadiliano  ya kukiri mashtaka kati ya mshitakiwa na DPP.

" Jamhuri tunaomba kubadilisha hati ya mashtaka na kwamba DPP ameridhia kufanya mabadiliko madogo katika hati ya mashitaka  kwa kumfutia mashitaka ya kutakatisha fedha " alidai Komanya.


Katika hati mpya ya mashitaka, mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matatu likiwemo la kuisababishia hasara Serikali ya dola za Marekani 980,000.


Ilidaiwa kwamba, shitaka la kwanza ni la kuongoza genge  la uhalifu, kuwa kati ya Oktoba 18 mwaka 2011 hadi Machi 9 2014 , ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  mshitakiwa huyo ambaye si mtumishi wa umma akishirikiana na watumishi wa umma, waliweza kutekeleza njama za hila ili kujipatia fedha .


Katika shitaka la pili ilidaiwa kati ya Januari 23   hadi Februari 10 mwaka 2014 katika benki ya Stanbic tawi la Kati ,wiaya ya Kinondoni na Benki ya UBL Ilala, Dar es Salaam, kwa nia ya udanganyifu, alijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania  (BOT), Dola za Marekani 380,000 na Dola 600,000.


Shitaka la tatu ni la kuisababishia serikali ya Tanzania Hasara  kwamba, katika tarehe hizo,  mshitakiwa huyo aliisababishia serikali hasara ya jumla ya Dola 980,000.


Baada ya kusomewa mashitaka hayo,  Hakimu alimtaka mshitakiwa huyo kutojibu mashitaka kwakuwa mahakama hiyo haina Mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi.


Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 4 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ,mshitakiwa amepelekwa maabusu.

No comments:

Post a Comment

Pages