Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Mawaziri nane wa kisekta wakioongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kesho tarehe 5 Oktoba 2021 wataanza ziara ya mikoa kumi kwa ajili ya kutoa matokeo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 920.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma leo tarehe 4 Oktoba 2021 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, ziara hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi kwa vile vijiji ambavyo wananchi wake walivamia maeneo ya hifadhi za misitu, mashamba na mifugo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, timu hiyo ya Mawaziri wanane itakayoambatana na Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta na Wataalamu wa wizara hizo itaanza kutembelea mikoa kumi kwa awamu ya kwanza na baadaye mikoa mengine 16 iliyosalia na kutimia jumla ya mikoa 26.
‘’Kuna baadhi ya hifadhi zimekosa sifa na serikali imeamua wananchi wabaki katika maeneo hayo kwa ajili ya kuendesha shughuli zao na halmashauri kwa kushirikiana na wataalamu zitakuja na zoezi la kupima na kuweka mpango wa matumizi bora ya ardhi ili waishi kwa amani’’ alisema Waziri Lukuvi.
Ameitaja mikoa ambayo Mwaziri hao watakwenda kuwa Dodoma watakayoanza katika wilaya ya Chemba, Singida, Manyara, Tabora, Mbeya, Morogoro, Geita, Mara, Dar es Salaam na Pwani.
Mawaziri watakaokuwa katika ziara hiyo ni kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Kilimo, Uvuvi na Mifugo, Mazingira, Utalii, Ulinzi na Maji.
‘’Katika ziara hii timu yetu ya Mawaziri itakutana na viongozi wa mikoa husika ili kupata taarifa mpya kuhusiaana na matumizi ya ardhi kwenye vijiji pamoja na kuwatangazia huruma ya rais ya kuwataka waliovamia maeneo ya hifadhi kubaki kuendesha shughuli zao bila bughudha’’. Alisema Lukuvi.
Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema, kuna baadhi ya maeneo kwenye vijiji hivyo itafanyika tathmini kwa lengo la kuanisha maeneo hatarishi na kusisitiza kuwa maeneo hatarishi wananchi hawatatakiwa kubaki.
Kwa muda mrefu kumekuwa na migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji vilivyokuwa maeneo ya hifadhi ambapo serikali iliombwa kuachia sehemu ya maeneo yaliyovamiwa ili wananchi wake kuendelea na shughuli zao jambo lililosababisha kuundwa kwa timu maalum ya Mawaziri wa Kisekta kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
No comments:
Post a Comment