HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 23, 2021

Mkoa wa Pwani wajipanga kukusanya bil 15.5. kodii pango la ardhi


Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Lucy Kabyemera akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari.

 

Na Asha Mwakyonde Dar es Salaam

KAMISHNA wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Pwani Lucy Kabyemera amewataka wananchi wa mkoa huo kulipa kodi ya pango la ardhi kwa kipindi hiki ili kuepuka kutozwa riba endapo watachelewa kulipa kodi hiyo.

Muda wa kulipa kodi hiyo bila riba ni kuanzia tarehe 1 Julai hadi tarehe 31 Disemba.

Pia amesema ndani ya kipindi hiki cha mwaka wa fedha 2021 - 2022 Mkoa wa Pwani wameanzisha kampeni inayohamasisha ulipaji kodi mapema inayosema ' Ujanja Kuwahi - Lipa Kodi ya Pango Ardhi mapema bila riba'.

Akizungumza mkoani Pwani jana Kabyemera amesema kodi ya pango la ardhi inalipwa kwa mujibu wa fungu la (33) la sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999.

Kabyemera ameeleza kuwa kwa mujibu wa fungu hilo kila mmiliki wa kipande cha ardhi anawajibu wa kulipa kodi hiyo kila mwaka. Aidha, ameeleza zaidi kuwa mmiliki anaweza kuilipa kwa mkupuo au kwa awamu.

" Leo nipo hapa kuelezea kuhusu ulipaji wa kodi ya  pango la ardhi na napenda kusisitiza zaidi umuhimu wa kulipa kodi hii mapema. Ukiwahi kulipa ndani ya muda kuanzia Julai hadi Disemba 31, unalipa bila riba lakini ukichelewa utatakiwa kulipa kodi sahihi na riba ambayo inayotozwa kila mwezi unaochelewa kulipa" amefafanua.

Ameongeza kuwa jinsi mmiliki wa kipande cha ardhi anavyoendelea kulimbikiza deni, hata yale malimbikizo yanaendelea kutozwa riba.

Kabyemera amefafanua kuwa mathalani mmiliki anadaiwa  shilingi 10,000 na akachelewa kulipa,  atatozwa labda 10100 na kwa mwezi unaofuata kama hatolipa basi riba kwa mwezi huo itatozwa kwa deni lote ambalo ni 10100 aliyotolea mfano.

" Nasisitiza na kuhimiza wananchi hususani mkoa wa Pwani kulipa kodi ya pango la ardhi mapema ndani ya kipindi hiki kilichowekwa ili kuepuka usumbufu na gharama zisizo za lazima" amesema Kabyemera.

Kamishna huyo Msaidizi amebainisha kuwa mkoa huo mwaka wa fedha wa 2020 - 2021 ulipewa leongo la kukusanya shilingi bil. 10.8  lakini hali halisi ya makusanyo hayo waliweza kukusanya  bil. 7.4 sawa na asilimia 69

"Mwaka huu wa fedha malengo yameongezeka  tunatakiwa kukusanya  bil.15.5  ambalo ni ongezeko la takribani bilioni 5. Tumejipanga kuhakikisha tunafikia lengo hili kwa kuhakikisha tunamfikia kila mmiliki wa ardhi ili tuhakikishe tunafikia au hata kuvuka malengo" amesema Kabyemera.

Ameeleza kuwa hadi kufikia Septemba 24 mwaka huu wameweza kukusanya kiasi cha shilingii bilioni 2 na kwamba kuanzia mwezi huu wa Oktoba wameanza utekelezaji wa kupita  nyumba hadi nyumba, kiwanja hadi kiwanja kwa lengo la kuhakikisha wanamfikia kila mmiliki aweze kulipa kodi ya pango la ardhi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

CHANGAMOTO

Kabyemera amesema changamoto  kubwa waliyonayo ni kushindwa kuwafikia wamiliki hususani katika maeneo ambayo hayajaendelezwa. Aidha ameeleza kuwa Sheria inawaruhusu kuchukua hatua kwa mtu ambaye halipi kodi hiyo.

" Tunaomba hata wale ambao hatuwezi kuwafikia kiurahisi wajisikie kuwajibika kulipa kodi hii bila shuruti. Wengine taarifa zao hazipo serikali za mitaa hususani wale ambao hawajaendeleza maeneo yao inakuwa ngumu kuwapata," amesema.

Ameongeza pia kuwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatekeleza zoezi la uhakiki wa kumbukumbu za wamiliki Ardhi wote. Hivyo wananchi watumie nafasi hiyo kuhakiki taarifa zao.

Kabyemera amesema  wakiwa na taarifa sahihi za mmiliki wa kipande cha ardhi ni rahisi kumfikia mmiliki huyo endapo kuna tatizo lolote kuhusiana na milki yake.

WITO

Kamishna huyo Msaidizi amewataka wamiliki kuhakikisha wanajaza madodoso yaliyosambazwa katika ofisi ya Serikali za Mitaa ambazo pia zinapatikana katika Ofisi za Ardhi Halmashauri na Ofisi za Makishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa zilizoanzishwa nchi nzima.

Kwa mujibu wa Kabyemera Mwananchi anaweza kujaza taarifa za Kiwanja au Shamba analomiliki sehemu yoyote nchini na kuziwasilisha katika Ofisi ya Mkoa yoyote iliyo jirani naye. Taarifa hizo zitafikishwa katika Ofisi husika.

Vilevile ameieleza kuwa wananchi wanaweza kupata taarifa kuhusu deni la kodi ya Pango la Ardhi katika Ofisi za Halmashauri na Makimishna wa Mikoa au kwa kutumia mitandao kwa kupiga namba 152*00# kupata maelejezo ya namna ya kulipia.

No comments:

Post a Comment

Pages