HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 23, 2021

Wafanyabiashara kariakoo: Rais Samia ingilia kati tusitolewe kama wamachinga

PATRICIA KIMELEMETA  

 

WAFANYABIASHARA wa ndani wa soko dogo la vyakula la Kariakoo wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro uliopo kati yao na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kupewa siku 10 kuondoka ndani ya soko ili kupisha matengenezo yanayodaiwa kuanza Novemba mosi mwaka huu.


Hatua hiyo imekuja baada ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Hassan Abbas kuwaita viongozi wa wafanyabishara hao Oktoba 19, Mwaka huu ofisi kwake na kuwaambia waondoke kabla ya Oktoba 30 ili kupisha matengenezo hayo huku akiwakabidhi kwa Ofisa Biashara aliyetambulika kwa jina la Thabit ili wakatafute maeneo mbadala ya kufanya shughuli zao ikiwamo eneo la Buza na Kigilagila.

Huvyo basi, wafanyabishara hao walitakiwa kufika Ofisi za Anatogro saa 4 kamili, Oktoba 20 ili waende kutafuta masoko hayo kwenye maeneo tajwa.

 Hata hivyo, viongozi wa fanyabishara hao waligoma kuondoka eneo hilo kwa madai kuwa, agizo la Rais Samia lilikua la kuwaondoa wafanyabishara wanaofanya shughuli zao katika maeneo yasiyo rasmi yakiwamo barabarani na sio kwenye eneo rasmi la soko hilo.

"Tumeshangazwa kuitwa na RAS, Hassan Abbas na kututaka tuondoke katika eneo la ndani ya soko dogo la kariakoo ili kupisha ujenzi ambao walituambia unaanza Novemba Mosi Mwaka huu, wakati mpaka sasa soko kubwa la Kariakoo lililoungua hatujui ukarabati wake unaanza lini, na wala ripoti ya kwanza kabla ya kuungua na ya pili baada ya kuungua hatujapata ili kujua chanzo chake," amesema Mwenyekiti wa Soko hilo, Hussein Omary.

Amemuomba Rais Samia kuingilia kati mgogoro huo kwa sababu wanaamini hauna baraka zake, bali wajanja wachache wanataka kutumia nafasi hiyo kuwaondoa ili kuficha madudu yaliyopo ndani ya soko hilo.

Amesema kuwa, soko la Kariakoo ni la Kimataifa, na la kihistoria pia, ndio maana wamekuwa wakipata wateja kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwamo wa Kenya, Msumbiji, Comoro,Uganda,Rwanda,Zambia,Malawi,Burundi hadi Jamhuri ya Demokrasia ya Congo(DRC),ili kununua bidhaa zilizopo bdani ya soko hilo jambo ambalo limewasaidia kupata fedha na Serikali kupata mapato yake.

"Hili soko ni la kihistoria, kwa sababu wakati mababu zetu wanapigania uhuru , baadhi ya vikao vilikuwa vikifanyika katika eneo hilo kwa kushirikisha wapagazi ambao walishirikiana na Mwalimu Julius Nyerere ili kupanga mipango yao, baadhi yao ni babu na baba zetu, sasa unapotangaza kuwaondoa wafanyabishara ndani ya siku 10 wakati tuna watoto wa kusomesha na familia zetu zinatutegemea tutapata wapi fedha za kutimiza majukumu ya familia zetu!", alihoji.
 
Amesema kitendo cha kutaka kuwapeleka kigilagila au buza kwa ajili ya kufanya shughuli zao ni sawa na kuwakomoa, hivyo basi wameomba uongozi wa juu wa Serikali kuungua kati mgogoro huo.
 
"Tunachoshangaa sisi ni kwamba, tupo eneo rasmi la biashara, ni ndani ya soko dogo, wateja wetu wanatoka nchi mbalimbali hadi wachina na mataifa mengine wanakuja kununua bidhaa zetu, ubapotupeleka Kigilagila au Buza nani anapajua?? Ni sawa na kuikosesha Serikali mapato," amesema Omary.
 
Ameongeza kuwa, wakati wa ukarabati wa soko la Kisutu na Magomeni, wafanyabishara walipewa eneo la pembeni ili waweze kuendelea na biashara zao huku ukarabati ukiendelea, lakini wanachoshangaa wao ni kuambiwa waondoke kabisa katika maeneo hayo huku wakikatazwa kutoongea na waandishi wa habari wala kuwapa taarifa ya kinachoendelea ndani ya soko hilo, jambo ambalo limewajengea mashaka.
 
Amesema kuwa, kama Serikali imepanga kufanya ukarabati inapaswa kuanza na soko kubwa lililoungua ili linapomalizika wafanyabishara hao wanapewa eneo la kufanya shughuli zao na kuendelea kufanya ukarabati wa soko dogo,kuliko kuwaamisha na kuwapeleka kigilagila.
 
Amesema kuwa, wamekuwa wakifanya bishara kwenye eneo hilo tangu miaka ya 70 na kulipa kodi halali ya Serikali ambapo baadhi yao wanalipa hadi Sh 700,000 kwa mwaka, kulingana na utaratibu waliopangiwa, lakini kinachowashangaza ni kuwaondoa ndani ya siku 10 bila ya kuwapa notisi wala kuwashirikisha kwenye suala hilo kama walivyofanya kwenye maeneo ya masoko mengine yakiwamo ya Kisutu na Magomeni ambapo wafanyabiashara walishirikishwa mwanzo hadi mwisho wakati wa ukarabati wa masoko hayo.
 
Amesema kuwa, hili kuondoa sintofahamu hiyo, wamemuomba, Rais,Makamu wa Rais, Dk.Philip Mpango, Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa na Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu kufika katika soko hilo kuzungumza na wafanyabishara hao ili waweze kueleza kinaendelea ndani ya soko hilo kwa sababu wanaamini kuwa,Ofisi ya Mkoa haiwezi kuwasaidia kwa sababu wao ndiyo wanaotaka kuwaondoa.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla, alisema "nipo ziarani, hao wafanyabiashara wa soko dogo siyo wamachinga, na hawahusiki na zoezi hili la wamachinga ila itakapotokea uamuzi wa ukarabati au ujenzi wa soko lao watajulishwa.
 
Naye Waziri wa Tamisemi Ummy Mwalimu alisema kuwa, "Nimelipokea na kumtaka RC anipe ufafanuzi kuhusu suala hili."

No comments:

Post a Comment

Pages