Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza kuhusu kilimohai kwenye kongamano hilo.
Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo.
Na Irene Mark
SERIKALI imeahidi kuanzisha kitengo maalum cha masuala ya kilimo ikolojia hai na kutenga bajeti yake kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023.
Ahadi hiyo imetolewa leo Oktoba 21.2021 na Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipofungua kongamano la pili la kimataifa la Kilimo Ikolojia na Kilimo hai linaloendelea jijini Dodoma.
Akizungumza mbele ya washiriki zaidi ya 300 kutoka ndani na nje ya nchi, Bashe amesema ni azma ya serikali kukiendeleza kilimo hai kwa kuwekeza kwenye mbegu asili.
Kuhusu mbegu Bashe amesema serikali kupitia Taasisi ya Utafiti ya Kilimo (TARI), itafanya utafiti wa mbegu asili na kuanzisha benki kubwa ya mbegu za asili kabla ya kuanzisha mfumo wa kusafisha mbegu hizo na kuzirudisha shambani.
“Mbegu za asili zikisafishwa vizuri mkulima akazitumia matokeo yake yatakuwa mazuri mno. Lakini pia mazao ya kilimo hai kwenye soko yanapata bei nzuri kuliko mengine ni mara 10 mpaka 20 ya bei ya mazao mengine,” amesema.
“Mwaka wa fedha 2022/23 wizara yetu itatenga bajeti kwa ajili ya kilimo hai kutokana na umuhimu wake kwa kuwa chakula ni tiba ya magonjwa mengi,” amesisitiza Bashe.
Naye Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, DK. Soud Nahodha Hassan, amesema kwa upande wa Zanzibar asilimia 60 ya kilimo kinachofanyika visiwani humo ni kilimo hai.
“Na sisi wizara tunajipanga kwa mwaka wa fedha tutaiweka bajeti ya kukiendeleza kilomo hai kwa sababu tunaona umuhimu wake, nimefarijika pia kuona huku bara napo watu wanakitaka sana kilimo hai,” amesema Dk. Soud.
Baadhi ya washiriki wa Kongamano hilo wamesema kauli ya naibu waziri huyo imewapa nguvu ya kuendelea na shughuli za kilimo hai kwa kuwa ipo nguvu ya serikali nyuma yao.
No comments:
Post a Comment