HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 12, 2021

Watoto, Vijana washauriwa kuitumia Mitandao ya Kijamii kwa manufaa


Mkurugenzi wa Shirika la Bright Jamii Initiative, Irene Fugara, akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani. 

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis akifurahia jambo pamoja na Mwenyekiti Baraza la Watoto Taifa, Nacy, katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani leo Dar Salaam.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Plan International Tanzania akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyofanyika katika Hoteli ya Kempnsk iliyopo jijini humo.
Wasichana wakiwa wanafuatilia jambo katika Maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini humo.

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Watoto na Vijana nchini wameshauriwa kuacha tabia ya kutumia vibaya mitandao ya kijamii au mifumo ya kidijitali badala yake wamehimizwa kuitumia katika fursa ya kujifunza na kufanya matangazo ya biashara pamoja na kuwasiliana na wateja.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis katika Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani.

Amesema kuwa mitandao hiyo iliyounganishwa katika mifumo ya kidijitali imetoa fursa nyingi kwa jamii kwani wanafunzi wanaweza kufanya mijadala ya kimasomo huku akibainisha matajiri wakubwa wamefanikiwa kwa kutumia mitandao ya kijamii hivyo vijana wametakiwa kuitumia kujikwamua kiuchumi kwenye shughuli wanazofanya.

" Dijitali imetoa fursa nyingi hata matajiri duniani wametumia ubunifu wao kupata utajiri kupitia mitandao ya kijamii ya Twitter, Instagram, Google na Facebook msiitumie katika matumizi yasiyo sahihi muitumie kufanyia masomo na vijana muweke matagazo ya biashara zenu," amesema Naibu Waziri Mwanaidi.

Amebainisha kuwa matumizi ya mitandao yasiyo sahihi yanachangia uwepo wa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo picha za ngono, vitisho pamoja na kuwarubuni vijana kushiriki vitendo viovu.

Ameongeza kuwa watoto wanatakiwa kutumia vyema elimu wanayopewa na sio kuvamia mambo yasiyoeleweka mitandaoni na kwamba tafiti kati ya watu nane kati ya 10 hutumia simu nyumbani huku asilimia 32 ya watoto waliofanyiwa vitendo vya uonevu mtandaoni wanakumbwa na msongo wa mawazo.

Amesisitiza kuwa kila mwaka Oktoba 11 Tanzania huungana na Umoja wa Mataifa (UN) kuadhimisha siku hiyo lengo likiwa kukumbushana  upatikanaji na ufuatiliaji wa haki za watoto hao na kwamba maadhimisho ya mwaka hu yamebeba kauli mbiu isemayo Kizazi cha Kidijitali Kizazi Chetu.

Amefafanua kuwa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) za mwaka jana zinaonyesha Watanzania milioni 51.2 wakiwemo watoto wanatumia simu huku zaidi ya watu milioni 1.5 wanatumia huduma za mitandao.

Ametoa rai kwa wazazi na walezi kufuatilia mienendo ya matumizi ya simu za watoto kwa kuzungumza nao waepuke matumizi yasiyo salama badala yake waitumie iwaletee manufaa,.

Ameishauri jamii kuendelea kujikinga na Ugonjwa wa Uviko 19 kwa kuendelea kuchanja chanjo ya ugonjwa huo pamoja kuzingatia kanuni za kujikinga ikiwemo kuvaa Barakoa na kutumia vitakasa mikono.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Bright Jamii Initiative, Irene Fugara amesema kuwa maadhimisho hayo hayatabaki kuwa tukio bali yatakuwa chachu ya kuendeleza  jitihada za wadau mbalimbali kuwawezesha watoto wa kike kushiriki katika ulimwengu wa kidijitali.

Mkurugenzi huyo amesema Kizazi Cha Kidijitali kitachochea upatikanaji wa fursa sawa kati ya mtoto wa kiume na kike na kwamba maadhimisho yamefanikishwa asasi mbalimbali ikiwemo Msichana Initiative, Mikono Yetu, Amani Girls, Religion for Peace, Shule direct na Global Peace Foundation Tanzania. 

Nae Mwakilishi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Save the Children, Besta amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha haki za mtoto wa kike zinalindwa ikiwemo haki ya kupata elimu na ulinzi dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Plan International Tanzania Paul Msato amesema wana mradi wa wasichana uliogawanyika katika makundi manne yakiwemo ya usawa katika kufanya maamuzi ya tija, usawa wa ushiriki, matumizi ya teknolojia, ushirikishwaji na utambuzi na kwamba tayari wamewazsha wasichana 20 kushika nafasi za uongozi kwenye mashirika.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Wanawake Nchini (UN Women), Odom Adu amesema wataendelea kuwatetea watoto wa kike na wanawake ili kuhakikisha wanapata haki zao za msingi.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu (UNFPA), Bibi Jacqueline Mahon amesema  wataendelea kushirikiana asasi nyingine kufanikisha malengo ya makundi ya watoto na wanawake.

Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Taifa, Nancy Kasembo ameiomba Serikali kuendela kuboresha huduma za kidijitali kwa watoto wa kike kwa kuwawezesha kupata vitendea kazi ikiwemo simu na kompyuta mpakato ili waeze kushiriki katika kujifunza.



No comments:

Post a Comment

Pages