HABARI MSETO (HEADER)


December 07, 2021

TARURA yawajengea uwezo Madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mfumo wa Kielektroniki wa Ushuru wa Maegesho

Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga akizungumza katika kikao hicho na kueleza kuwa mabadiliko yaliyofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wakala huyo yana tija kwa wananchi wa hali ya chini.
 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mjijini Tanzania (TARURA) imetoa elimu ya kuwajengea uwezo Madiwani  wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ilala  juu ya matumizi ya Mfumo wa Kieletroniki wa Ushuru wa Maegesho (TeRMIS) ambao utaanza kutumika tena Disemba Mosi mwaka huu katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mwanza, Singida na Dodoma.

Akifungua kikao hicho jijini humo Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Charangwa Makwiro amesema mfumo huo wa ukusanyaji mapato ni sahihi katika kuzuia mapato yaliyokuwa yanapotea pamoja na kuziba mianya mbalimbali iliyosababisha kupotea kwa mapato hayo.

Amebainisha, kushirikishwa kwa Madiwani na viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama wa jiji hilo ni muhimu kwa kuwa hao ni viungo muhimu walio karibu na wananchi hivyo wanategemea matokeo chanya mara baada ya mkutano huo katika uwezeshaji wa kufanikiwa kwa mfumo huo.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi, Geofrey Mkinga  amesema matumizi ya mfumo huo ni katika kwenda na azma ya Serikali ya kuhama kutoka mfumo wa analojia kwenda kidigitali hasa katika ukusanyaji wa mapato na baada ya changamoto kadhaa kutokea na kusimamishwa kwa mfumo huo kwa muda marekebisho yamefanyika na elimu zaidi imetolewa kwa Umma kupitia makundi mbalimbali yakiwemo vongozi na waandishi wa habari ili wananchi waweze kufikiwa na taarifa hizo na kwenda sambamba na mfumo huo wa ukusanyaji mapato.

Kuhusiana na mabadiliko yaliyofanyiwa kazi ni pamoja na kupunguzwa kwa adhabu ya 30,000 na adhabu ya mara mbili ya kutofanya malipo baada ya siku saba na kuongezwa kwa siku 14 za malipo na ndani ya siku hizo mteja atakumbushwa mara mbili huku watumiaji wa mitandao ya simu  wakikumbushwa kufanya malipo na kampuni hiyo.

Mhandisi Mkinga amesisitiza kuwa mabadiliko hayo yamepunguza tozo ya siku kutoka shilingi 4500 hadi 2500 na tozo kwa saa ikibaki Sh 500 huku taarifa za wapi mteja alipaki zitabaki kuwa siri kwa usalama wa mfumo na watumiaji wake.

Nae,Meneja wa TEHAMA kutoka TARURA, Stanley Mlula amesema wamebadilisha mfumo wa ulipaji tozo zitabaki kama zilivyo na hiyo ni kwa malengo ya kuzuia kupotea kwa mapato kwa kuzuia malipo ya fedha mbichi (cash) na kutumia mfumo wa malipo ya 'control number' ambapo wateja watalipa kwa simu na benki (NMB na CRDB.)

Mstahiki Meya wa Jiji hilo, Omary Kumbilamoto ameipongeza TARURA kwa kupitia changamoto hizo kwa kushirikiana na Serikali (TAMISEMI) na wanaamini mfumo huo utafanya kazi kwa mafanikio makubwa hasa katika ukusanyaji wa mapato.

Meya Kumbilamoto amefafanua kuwa ni muhimu kwa Wakala hiyo kuwashirikisha madiwani na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika masuala yanayohusu jamii kutokana na muunganiko muhimu na wa moja kwa moja wa viongozi hao na wananchi.


No comments:

Post a Comment

Pages