HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 26, 2022

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI ARIDHISHWA NA UJENZI WA DARAJA LA KITENGULE


Naibu waziri wa ujenzi na uchukuzi mhandisi Godfrey Kasekenya na timu yake wakikagua ujenzi wa daraja la kitengule.

Na Lydia Lugakila, Karagwe


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amekagua daraja la Kitengule linalounganisha Wilaya ya Misenyi na Karagwe mkoani Kagera litakalofungua fursa ya shughuli za kilimo cha miwa mara litakapokamilika.


Mhandisi Kasekenya amesema kuwa ujenzi huo umefikia hatua nzuri ambapo amemtaka mkandarasi kukamilisha daraja hilo ifikapo mei 26 mwaka huu.


"Kwa upande wa daraja nimejionea umekamilika kwa asilimia 97.4 na tayari tumehakikisha kuwa limeishaanza kutumika kwa kiasi fulani magari sasa yanapita nimpongeze sana mkandarasi kwamba sasa tunaweza kuona matunda, miwa ilikuwa ishaanza kuharibika kwa kuwa ilikuwa ngumu sana kusafirisha sasa tumewapa muda muongeze mpaka mei 26 mwaka huu daraja liwe limekamilika na kukabidhiwa" alisema mhandisi Kasekenya.


Naibu waziri huyo amesema kuwa daraja hilo limejengwa maalum kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa miwa, kupunguza gharama za uzalishaji wa sukari katika kiwanda cha sukari Kagera kwa sababu ya kupunguza umbali uliokuwepo katika usafirishaji.


Ameongeza kuwa katika upande wa wilaya ya Karagwe kulikuwa na mashamba mengi ya miwa lakini mzunguko wa uchukuaji miwa na kuileta katika kiwanda cha miwa ilikuwa uzunguke takribani kilometa 60.


Aidha amesema kukamilika kwa daraja hilo barabara za kuzunguka daraja hilo zenye urefu wa kilometa 18 zitajengwa kwa kiwango cha rami huku akiona kuwa Kuna haja ya kuunganisha barabara toka mto Kagera mpaka barabara ya Bunazi kilometa 25 na kutaka mshauri kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili  wananchi wafanye shughuli zao bila vikwazo.


Naye Lebahati Emmanuel ambaye ni Meneja mashamba Kitengule amesema uwepo wa daraja hilo ni msaada mkubwa kwani miwa mingi imekuwa ikipungua kiwango kutokana na changamoto ya usafirishaji huku akiishukuru serikali kwa maono yenye kuinua uchumi Kagera na taifa kwa ujumla.


Aloyce Charles na Avitus wananchi wa maeneo hayo wanasema daraja dogo lililokuwepo mwanzoni lilikuwa hatari kwa maisha yao kwani halikuwa salama sasa uwepo wa daraja jipya ni fursa kiuchumi na usalama wa maisha yao.


Kukamilika kwa daraja hilo ifikapo mei 26 mwaka huu kiasi cha shilingi bilioni 25 na milioni 500 zitakuwa zimetumika huku serikali ikitaraji kuzalisha sukari hadi kuuza kwa wingi maeneo mengi nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages