Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women and Youth Foundation, Mwanaisha Mndeme akizungumza wanakina mama na vijana kuhusu masuala sheria na ukatili wa kijinisia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Women and Youth Foundation, Mwanaisha Mndeme, akitoa taulo za kike wa watoto wa Kituo cha Watoto Yatima cha Hisani kilichopo wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Women and Youth Voice Foundation, imeanzisha program ya kutoa elimu kuhusu sheria na ukatili wa kijinsi kwa wanafunzi wa shule za msingi wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Mwanaisha Mndeme wakati akizungumza na gazeti hili, ambapo aliweka bayana kuwa lengo kuu la wao kuanzisha taasisi hii ni kusaidia jamii ya Kitanzania kupata ufahamu wa masuala ya kisheria na ukatili wa kijinsia.
Mndeme amesema kwa siku za karibuni kasi ya jamii kutojua sheria na matukio ya ukatili wa kijinsia yamekuwa yakiongezeka hivyo njia sahihi ya kukabiliana na changamoto hiyo ni kutoa elimu kuanzia ngazi ya shule za awali, msingi na sekondari.
Mkurugenzi huyo amesema katika program hiyo wanatarajia kufikia wanafunzi wa jinsi zote katika shule zaidi ya tano wilayani humo na kwamba mipango yao ni kuwafikia Watanzania wote.
“Tunatarajia kuanzia wiki ijayo, tutaanza kutekeleza program yetu ya kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria na ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa shule takribani tano ambazo ni Kigamboni, Ufukoni, Vijibweni, Kisiwani na Mji Mwema,” amesema.
Amesema imani yao kupitia mafunzo hayo kwa wanafunzi wa shule za msingi, wataweza kubainisha mitazamo kwa kundi hilo ambalo limekuwa likikumbana na changamoto hasa ya ukatili wa kijinsia.
Mkurugenzi huyo amesema katika mafunzo hayo watashirikiana na maofisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri jambo ambalo litaongeza uzito.
Mndeme amesema pia watatumia mafunzo hayo kuwapa wanafunzi motisha na kujiamini ili waweze kutimiza ndoto zao, ambapo wengi wao zinaishia njiani.
“Kuna changamoto kubwa ya makuzi kwa watoto wetu, hivyo naamini kupitia program hii tutaweza kuwafanya wanafunzi kuishi katika ndoto zao,” alisema.
Aidha, mkurugenzi huyo alitoa rai kwa wadau mbalimbali kuwapa ushirikiano ili waweze kufikia malengo yao ya kufikia kila pande ya nchi hasa vijijini ambapo changamoto ya masuala ya sheria na ukatili wa kijinsia vipo.
Mndeme amesema taasisi
yao inaamini iwapo kila mdau atashiriki katika utoaji elimu kuhusu sheria na
madhara ya ukatili wa kijinsia ni dhahiri kuwa jamii itabadilika na kuishi kwa
upendo na amani.
No comments:
Post a Comment