HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 24, 2022

Milioni 300/- za Uviko zaongeza mtandao wa maji Ruangwa


Meneja wa Mamlaka ya Maji Ruangwa mjini, Yohana Matimbwi akipanda juu ya tenki la maji Ruangwa mjini.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Ruangwa mjini, Yohana Matimbwi na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Mhandisi Lawrance Mapunda wakiangalia maji yakiingia kwenye tenki la maji.
Mwananchi wa kijiji cha Nanganga, Fatuma Lukanga akijitishwa ndoo ya maji.
Mwananchi wa kijiji cha Nanganga, Fatuma Lukanga akiwa amebeba ndoo ya maji mita tano kutoka nyumbani kwake.

 

Na Selemani Msuya, Ruangwa 

 

SHILINGI milioni 313 za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, zilizotolewa na Serikali na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), zimefanikiwa kuongeza mtandao wa maji wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Fedha hizo Sh.milioni 313 ni kati ya Sh.trilioni 1.3 za mkopo usio na riba zilizotolewa na IMF ambapo Serikali imetoka mradi mmoja kwa kila jimbo.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Mamlaka ya Maji Ruangwa mjini, Yohana Matimbwi wakati akizungumza na waandishi wa habari walitembelea miradi mbalimbali inatokelezwa kwa fedha za ustawi.

Matimbwi amesema Ruangwa mjini mtandao wa maji ulikuwa unapatikana katika baadhi ya maeneo, hivyo mradi huo utaongeza asilimia ya upatikanaji wa maji kutoka 52 na watu 3,120 watanufaika.

Meneja huyo amesema katika mradi huo mamlaka ambao unagharimu Sh.milioni 313 wanakarabati tenki la maji lenye ujazo wa lita 135,000, kuongeza mtandao wa maji wa kilomita 11.8 na kujenga vituo vya maji na hadi sasa kazi imekalimika kwa asilimia 93.

“Mradi huu wa kuongeza mtandao wa maji katika mji wa Ruangwa umefikia asilimi 93 ya utekelezaji ambapo wa wananchi 3.120 watanufaika katika kata zote za mjini kama Kilimani Hewa,” amesema.

Meneja huyo amesema kupitia mradi huo na miradi mingine wantarajia Ruangwa kufikia lengo la upatikanaji maji kwa asilimia 95 ifikapo 2025.

Matimbwi amesema mamlaka inamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kuwapatia fedha za kutekeleza miradi ya maji, ili kuwaondolea wananchi adha hiyo.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Ruangwa, Lawrence Mapunda amesema mamlaka hiyo imedhamiria kumtua ndoo mama kichwani kwa kufikisha maji safi na salama bombani.

Mapunda amesema changamoto ya maji wilayani hapo imekuwa ikisababisha madhara kwa wananchi, hivyo wanahangaika kutafuta vyanzo kila kukicha ili kuwapatia wananchi maji ya uhakika.

“Tunachokifanya sisi RUWAS ni kuhakikisha tunatekeleza Sera ya Taifa ya Maji ambayo inataka kila mwananchi kuchota maji katika umbali usiozidi mita 400, naamini tutafanikiwa kwani kazi inaendelea,” amesema..

Naye mwananchi Fatuma Lukanga wa kijiji cha Nanganga amesema ujio wa RUWASA umesaidia kuwanusuru na majanga ya kushambuliwa na wanyama kama Mambo na Boko.

“Ujio wa maji umebadilisha maisha yetu, tunamshukuru Rais Samia kuwawezesha RUWASA kutuletea maji safi na salama,” amesema.

Dickson Omary amesema ujio wa maji safi na salama kijijini kwao kumewaondolea adha ya kupata magonjwa kama kichocho, kipindupindu na mengine.

Aidha, Omary ameomba RUWASA kuweka mazingira mazuri ya kulinda vyanzo vya maji, ili viweze kuwa endelevu.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa amesema katika mkoa huo wanahudumia vijiji 524 ambapo hadi sasa asilimia ya upatikanaji maji ni 66.

Mhandisi Lubasa amesema Lindi imepata Sh.bilioni 2.6 za ustawi ambazo zinatekeleza miradi sita kwenye wilaya tano za mkoa huo.

“Kupitia fedha za ustawi tunatarajia hadi mwezi Julai tutaongeza zaidi ya asilimia tano ya upatikanaji wa maji, hivyo kuwafikia watu 140,000 ambapo watu 40,000 watakuwa wapya,” amesema

Lubasa amesema miradi yote ya ustawi inayotekelezwa hadi sasa imefikia zaidi ya asilimia 40, hivyo ni imani yake dhamira ya RUWASA kumtua ndoo mama kichwani itatimia.

Amesema kupitia miradi ya ustawi na mingine wanatarajia ifikapo 2025 Lindi maji yatakuwa yanapatikana kwa asilimia 85.

No comments:

Post a Comment

Pages