HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 13, 2022

Mwongozo wa sifa, tuzo kitaaluma waja


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Herman Sedoyeka, akizungumza wakati akifungua  mkutano wa wadau wa elimu kujadili Mwongozo wa Kitaifa wa Ulinganifu wa sifa na Tuzo za Kitaaluma ili kumuwezesha mtanzania kujiendeleza kielimu au kupata ajira bora nje ya nchi. Uzinduzi huo ulifanyika Dar es Salaam leo Aprili 13,2022. (Picha na Francis Dande).

 

Baadhi ya wadau wa elimu wakiwa katika mkutano huo.

Mkamu Mkuu Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akiwa katika mkutano huo.

Picha ya pamoja.

Na Irene Mark

SERIKALI ipo kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya rasimu ya Mwongozo wa Kitaifa wa Ulinganifu wa sifa na Tuzo za Kitaaluma ili kumuwezesha mtanzania kujiendeleza kielimu au kupata ajira bora nje ya nchi.

Mwongozo huo (Tanzania Qualification Framework), utatumika kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na hata nje ya Afrika.

Akizungumza Dar es Salaam leo Aprili 13,2022 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa elimu kujadili muongozo huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Herman Sedoyeka, aliwapongeza wadau hao na kusema anaamini utapatikana mwongozo bora.

Sedoyeka amesema mwongozo huo unalenga kuwianisha sifa za kitaaluma hapa nchini huku ukiwianisha viwango, maarifa, ujuzi na umahiri unaotarajiwa au unaohitajika kwa soko la ajira kwenye mfumo wa elimu na mafunzo ndani na nje ya mipaka ya nchi.

“Ndugu zangu ikumbukwe kwamba mwongozo huu umeandaliwa kutokana na ukweli kwamba Tanzania yetu haijawahi kuwa na mwongozo huu.

“...Mifumo ya kwanza ya Kitaifa ya Ulinganifu wa sifa na Tuzo za Kitaaluma (NQF) ilianzishwa nchini Uingereza katikati ya miaka ya 1980 na hii ilileta shauku zaidi kwa nchi nyingi kuandaa miongozo yake, sababu ni kuboresha uwazi na kuonesha umuhimu wa ulinganifu wa sifa na tuzo za kitaaluma pia kufungua fursa za kupata elimu na ajira kutoka pande tofauti bila vipingamizi,” amesema Sedoyeka.

Amesema nchi zinaangalia muktadha wa kielimu, kijamii, kiuchumi na kisiasa pia.

“Miongozo mingi inayoandaliwa inafuata ajenda ya Elimu ya mwaka 2030 na SDG namba nne ambalo linakuza elimu jumuishi na yenye usawa pamoja na fursa za kujifunza stadi za maisha.

“...Mifumo au miongozo hii inategemea matokeo ya ujifunzaji hivyo kuchangia moja kwa moja kwenye utekelezaji wa lengo hili,” amesisitiza Sedoyeka.
 
Mratibu wa mkutano huo, Dk. Noel Mbonde ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundistadi, amesema mwongozo huo ni nyaraka muhimu ambayo haijawahi kiwepo kabla na baadanya uhuru wa nchi yetu.

“Hii sasa itasaidia kuonesha uwezo wa kitaaluma wa watanzania ndani lakini zaifi nje ya nchi na kutuwezesha kufanyakazi huko ndio maana leo tunao wanataaluma wabobezi wote hawa wataunganisha uwezo na maarifa yao kuwezesha kupatikana kwa nyaraka hiyo muhimu,” amesema Dk. Mbonde.

Mkutano huo wa siku moja umewakutanisha Wakurugenzi na maofisa kutoka Wizara ya Elimu, Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu, Wakuu wa vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi au wawakilishi wao.

Wengine waliohudhuria ni Wakuu na Wakurugenzi wa Mashirika yote yaliyopo hapa nchini, Wathibiti ubora wa Elimu katika ngazi zote, Wawakilishi wa UNESCO, Wakuu wa vyuo vyote vya Elimu- LITI, Wawakilishi wa Shule za Sekondari, Wawakilishi wa Shule za Msingi, Wawakilishi wa Wanafunzi wa shule za Sekondari na shule za msingi na Wadau wa elimu.

No comments:

Post a Comment

Pages