HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 24, 2022

RUWASA kumaliza kero ya maji Lionja, Mchangani

 

 Mhandisi Milembe Magembe wa RUWASA Nachingwea akikata nguzo mbele ya mafundi wanaojenga Mradi wa Maji Mchangani wilayani hapo.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea, Mhandisi Sultan Ndoliwa, akiwaonesha waandishi wa habari maeneo ambayo yatanufaika na Mradi wa Maji Mchangani.
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa akiwaelezea waandishi wa habari namna ambavyo RUWASA mkoani hapo imetekeleza miradi ya maji ukiwemo wa Ustawi.

Mafundi wanajenga Mradi wa Maji Mchangani wilayani Nachingwea wakiendelea na kazi.


Na Selemani Msuya, Nachingwea

 

MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Nachingwea imetumia  Sh.milioni 784 kumalizi kero ya maji katika vijiji vya Lionja na Mchangani wilayani humo.

Kero ya maji Mchangani inakwisha baada ya Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza mkopo usio na riba wa Sh.trilioni 1.3 za Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kutumika kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.

Akizungumzia mradi huo wa ustawi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nachingwea Mhandisi Sultan Ndoliwa, amesema wanatekeleza miradi miwili katika vijiji vya Lionja na Mchangani ambapo wananchi wake wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji safi na salama.

Mhandisi Ndoliwa amesema Mradi wa Maji Mchangani unagharimu Sh.475 ambapo utakuwa na vituo nane vya kuchotea maji, mtandao wa bomba kilomita 14.5, ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 100,000 na kunufaisha watu 3,682.

Meneja huyo amesema pia RUWASA wanajenga Mradi wa Maji Lionja kwa fedha za ustawi, ambao unagharimu Sh.milioni 309 na utaweza kunufaisha watu 3,549, kujenga vituo tisa na usambazaji wa bomba.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unaenda na Sera ya Taifa ya Maji ambayo inataka kila mwananchi kuchota maji katika umbali usiozidi mita 400.

“Miradi hii ya fedha za ustawi imeelekezwa katika vijiji ambavyo vina changamoto kubwa ya maji, hivyo imani yetu ikikamilika wananchi hao watanufaika na kuwafanya wajishughulishe na kazi za kiuchumi na maendeleo,” amesema.

Amesema RUWASA Nachingwea imedhamiria kumtua ndoo mama kichwani kwa kumfikishia maji bombani nyumbani, hivyo pamoja na miradi ya ustawi wanaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ambayo itawawezesha wananchi wote wanapata maji safi na salama.

Mhandisi Ndoliwa amesema wanamshukuru Rais Samia kuwapatia fedha za miradi ya ustawi na kumuomba aongeze fedha zaidi katika wilaya hiyo ili lengo lao la kufikia asilimia 85 ya maji vijiji linafanikiwa.

Naye Msimamizi wa Mradi wa Maji Mchangani wilayani Nachingwea, Mhandisi Milembe Magembe amesema utekelezaji wa mradi huo wa ustawi umeenda vizuri kutokana na ushirikiano anaopata kutoka  RUWASA na mafundi.

Mhandisi Magembe ametoa wito kwa wahandisi wenzake kusimamia miradi kwa uadilifu na nidhamu, ili kuhakikisha dhamira ya Rais Samia kumtua ndoo mama kichwani inafanikiwa.

“Sisi wanawake tunaweza na ushahidi ni huu hapa ambao nimeonesha mimi hapa Mchangani, mradi unakaribia kumalizika,” amesema.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa amesema katika mkoa huo wanahudumia vijiji 524 ambapo hadi sasa asilimia ya upatikanaji maji ni 66.

Mhandisi Lubasa amesema Lindi imepata Sh.bilioni 2.6 ambazo zinatekeleza miradi sita kwenye wilaya tano za mkoa huo.

“Kupitia fedha za ustawi tunatarajia hadi mwezi Julai tutaongeza zaidi ya asilimia tano ya upatikanaji wa maji, hivyo kuwafikia watu 140,000 ambapo watu 40,000 watakuwa wapya,” amesema

Lubasa amesema miradi yote ya ustawi inayotekelezwa hadi sasa imefikia zaidi ya asilimia 40, hivyo ni imani yake dhamira ya RUWASA kumtua ndoo mama kichwani itatimia.

Amesema kupitia miradi ya ustawi na mingine wanatarajia ifikapo 2025 Lindi maji yatakuwa yanapatikana kwa asilimia 85.

Naye Mhandisi Daudi Omary kutoka Kampuni ya Ukandarasi ya Katon Traders amesema fursa hiyo ya ujenzi wa mradi wa ustawi wanaitekeleza kwa viwango vizuri, ili kuonesha thamani ya fedha iliyotumika na kudumu kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Fundi Juma Masanja, amesema mradi huo wa ustawi umemuwezesha kuhudumia familia yake kwa uhakika na kumuomba Rais Samia atoe miradi mingine ili vijana wapate kazi za kufanya.

“Hizi kazi zina umuhimu kwa vijana, mfano mimi nimetoka Mwanza hadi hapa Nachingwea kufanya kazi ya ujenzi, naomba kazi hizi ziwe nyingi,” amesema.

Fundi Meshack Katias ambaye pia ni mkazi wa Nachingwea amesema mradi huo anaujenga katika ubora mkubwa kwa kuwa utamnufaisha yeye na ndugu zake.

“Hapa Mchangani upatikanaji wa maji ulikuwa wa shida, hasa wakina mama wajawazito na wanafunzi, ila naamini kuanzia sasa tutakuwa tunaishi kwa amani kwani maji ni ya uhakika. Namuomba Mwenyezi Mungu ampe nguvu mwaka 2025 tutamlipa kwa kumchagua tena,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Pages