Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Tunduru, Mhandisi
Silvia Ndimbo, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa Kampuni ya Ujenzi ya
Civito, Mhandisi Stanley Mlelwa kuhusu ujenzi wa tenki la maji la Daraja
Mbili wilayani hapo.
Baadhi ya mambomba ambayo yamesambazwa katika vijiji vya Daraja Mbili na Kazamoyo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Na Selemani Msuya, Tunduru
WAKALA
wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma imetumia zaidi ya Sh.milioni 974.8 kumaliza kero ya maji
katika vijiji vya Kazamoyo na Daraja Mbili ifikapo mwishoni mwa mwezi
Mei, mwaka huu.
Hayo
yamesemwa na Kaimu Meneja wa Ruwasa wilayani Tunduru, Mhanmdisi Silvia
Ndimbo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii ambaye alitembelea
miradi ya maji inayotekelezwa kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa
Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Miradi
hiyo ya maji inatekelezwa kupitia fedha za mkopo usio na riba kutoka
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Sh. trilioni 1.3 zilizokopwa na
Serikali ya Tanzania.
Mhandisi
Ndimbo amesema Tunduru imepata miradi miwili ambayo inatekelezwa katika
majimbo mawili ya Tunduru Kusini na Kaskazini kwa fedha za ustawi.
Kaimu
meneja huyo amesema miradi hiyo itagharimu zaidi ya Sh. milioni 974
ambapo Mradi wa Maji Kazamoyo unagharimu Sh.milioni 476.5 na Daraja
Mbili Sh.milioni 498.3 ambapo kazi zote zipo katika hatua nzuri.
“Kazi
ambazo zinatekelezwa ni uchimbaji wa mitaro, ulazaji wa mabomba ambapo
hadi sasa kilomita 16 kati 18 bomba limesambazwa, ujenzi wa vituo saba,
tanki na nyumba ya mitambo,” amesema.
Kaimu
meneja huyo amesema miradi hiyo inayotekelezwa na Kampuni ya Ukandarasi
Civito itaongeza asilimia ya upatikanaji wa maji wilaya hiyo hadi
kufikia asilimia 68 na matarajio yao kufikia asilimia 74 ya upatikaji wa
maji mwisho wa mwaka huu.
“Ipo
miradi ya Mtuwesi, Senene, Basiburu, Kazamoyo, ufungaji wa pampu katika
vijiji 20 na uchimbaji wa visima 18, ambapo matarajio yetu ni ifikapo
2025 tutakuwa tumefikia asilimia 85,” amesema.
Amesema
Tunduru ina changamoto kubwa ya vyanzo vya maji na kwamba asilimia
kubwa ya maji yanayotumika yanatokana na visima, hivyo wanaomba Serikali
Iendelee kutoa fedha za miradi ya maji.
Mhandisi
Ndimbo amesema anaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kuipatia RUWASA fedha za miradi ya maji hali ambayo
itafanikisha kauli mbiu yao ya maji bombani hivyo kumtua ndoa mama
kichwani.
Kwa upande wake
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Rebman Ganshonga amesema
watahakikisha wanashirikiana na mameneja wa RUWASA wilaya kufanikisha
lengo la upatikanaji maji vijiji kwa asilimia 85 ifikapo 2025.
Mhandisi
Ganshonga amesema RUWASA inatambua umuhimu wa upatikanaji wa maji safi
na salama, hivyo fedha inayopatikana inatumika kama ilivyopangwa, ili
kuweza kumtua ndoo mama kichwani.
"Sisi RUWASA tunaposema kumtua mama ndoo kichwani tunamaanisha maji yatoke bombani na hili limetimia kwa asilimia nzuri,"amesema
Aidha,
Mhandisi Ganshonga amesema katika kuhakikisha maji yanapatikana kwa
uhakika wanashirikiana na wadau wote kutunza mazingira.
Naye
Mkandarasi kutoka Kampuni ya Civito, Mhandisi Stanley Mlelwa amesema
miradi hiyo itakamilika kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wa vijiji
vya Kazamoyo na Daraja Mbili ambayo hawajawahi kutumia maji ya bomba
tangu kupata uhuru wanayapata.
"Miradi hii miwili tunaitekeleza kwa ufanisi mkubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa wakati,"amesema.
No comments:
Post a Comment