HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 07, 2022

VIONGOZI WA DINI WATAKA WANAWAKE WAKISHIRIKISHWE NGAZI ZA MAAMUZI

 

Na Jasmine Shamwepu, Dodoma

VIONGOZI wa dini nchini wameiomba serikali kuweka mfumo rasmi ambao utawezesha kundi la wanawake kushirikishwa katika uongozi na ngazi za maamuzi kama ilivyo kwa wanaume bila kuwepo na ubaguzi au uzalilishaji wa kijinsia.

Askofu Method Kilaini, kutoka baraza la maaskofu katoliki Tanzania (TEC), alitoa ombi hilo alipokuwa akifungua mdahalo wa kitaifa kuhusu nafasi ya viongozi wa dini katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na ngazi za maamuzi.

Mdahalo huo umeandaliwa na shirika la Wanawake katika sheria na Maendeleo Barani Afrika(WiLDAF).

Kilaini, alisema ili nchi yoyote ipige hatua ni lazima kuwashirikisha wanawake katika maamuzi na mipango ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Alisema kwa mujibu wa takiwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 idadi ya wanawake nchini ni asilimia 51 hivyo kundi hilo kubwa halipaswi kutengwa katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi.

“Ili kundi hili la wanawake kupata ushiriki wa uhakika kwenye uongozi na ngazi za maamuzi lazima kuwepo na mfumo rasmi utakao saidia kundi hili kuingia katika uongozi bila kuwepo kwa upendeleo au ubaguzi.

“Ni lazima kuwepo na sheria na sera ambayo itaelekeza kuwa kundi hili ni lazima kuwepo katika ngazi na maamuzi bila kutegemea viti maalum ili kuweza kufikia usawa wa kweli kama ambavyo hata vitabu vya dini vinaelekeza kuhusu usawa kwa mwanaume na wanawake”alisema

Aidha, alisema utafiti unaonyesha kuwa ipo sababu ya kuwepo kwa sheria mahususi itakayo simamia suala hilo ili kuleta uwiano mzuri katika nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

“Katika nafasi za uongozi kama vile mwenyeviti wa mitaa, madiwani bado zipo chini lakini pia hata katika ubunge idadi bado ipo chini sana pamoja na uwepo wa viti maalum”alisema Askofu Kilaini

Anna Kulaya, mratibu wa kitaifa wa shirika la wanawake katika sheria na maendeleo Afrika (WiLDAF) alisema lengo ka mdahalo huo ni kujadilina na viongozi wa dini mchango wao katika kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi na ngazi za maamuzi.

Kulaya, alisema viongozi wa dini wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha jamii kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa kundi la wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi.

“Ipo haja ya kuwepo kwa mfumo rasmi ambao utawezesha wanawake kushiriki katika uongozi na ngazi za maamuzi badala ya kuendelea kutegemea vitimaalum ambavyo navyo vinawanyima kuwa na fedha za mfuko wa jimbo.

“Ni lazima tuwe na mfumo ili jinsia zote mbili kushiriki katika ngazi za maamuzi”alisema Kulaya  

Shekhe wa mkoa wa Dodoma Mustafa Rajabu, alisema ushiriki katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi kwa wanawake ni jambo la muhimu kwani mungu aliumba watu wote katika usawa.

“Vitabu vya dini vinaonyesha pia mwanaume na mwanamke mungu amewaumba katika usawa lazima tuwape wanawake nafasi za maamuzi ili waje na mtazamo wa tofauti na wanaume ili tupate radha zote mbili”alisema

Alisema, Tanzania ni moja ya Taifa ambalo mungu kaliwezesha kupata nafasi ya kuonja radha ya uongozi wa Rais mwanamke ambaye amekuja na mtizamo tofauti na wanaume ambao umeongeza kasi ya kuleta maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Pages