Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora Rashidi Magope (aliyesimama) akiwa katika picha ya pamoja na Makamu Mwenyekiti wa halmshauri na Viongozi wengine wa halmashauri hiyo katika moja ya mikutano ya baraza la madiwni, wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya hiyo John Pallingo na aliyekaa mwishoni kushoto ni Mwenyekiti wa CCM wilayani humo Anna Chambala.
Na Lucas Raphael, Tabora
HALMASHAURI ya Wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imefanikiwa kutekeleza miradi ya zaidi ya sh bil 6 katika kipindi cha mwaka mmoja wa serikali ya awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo John Pallingo alipokuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana katika wilaya hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja wa utawala wa Rais Samia katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Alisema katika kipindi cha siku 365 ambazo Rais amekaa madarakani wilaya hiyo imepata mafanikio makubwa katika sekta ya elimu, afya, barabara na maji kutokana miradi iliyotekelezwa kwa fedha za Uviko 19.
Alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita ilitoa zaidi ya sh bil 2.7 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 98 katika shule za msingi na sekondari kupitia fedha za Uviko-19.
Alibainisha kuwa fedha hizo zimewezesha kutekelezwa kwa ujenzi wa shule ya sekondari ya Kata ya Nyahua na kumalizia vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja miundombinu ya sekta ya elimu imeboreshwa kwa kiasi kikubwa jambo lililopelekea kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi na ufaulu kwa asilimia kubwa.
Akielezea mafanikio ya sekta ya afya, DC Pallingo alisema walipokea bil 2.6 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya afya katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa jengo la Wazazi (Martenity Complex) na Kituo cha Afya Tutuo .
Aliongeza kuwa walikamilisha ujenzi wa zahanati 2 za Mwamayunga na Kidete, ujenzi wa jengo la dharura, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la upasuaji, wodi 2 za upasuaji katika hospitali ya wilaya na miradi ya barabara ambayo imekuwa na tija kubwa katika wilaya na jamii kwa ujumla.
Alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha nyingi zilizowezesha kuboreshwa kwa huduma za jamii katika sekta mbalimbali wilayani humo katika kipindi kifupi tu, huku akiahidi kuwa wataendelea kuchapa kazi kwa weledi mkubwa.
No comments:
Post a Comment