HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 20, 2022

WATANZANIA WATAKIWA KUTEMBELEA MICHORO YA MIAMBANI


Muhifadhi na Mkuu wa Kituo cha Michoro ya Kondoa Irangi, Bw. Zuberi Mabie, akionesha michoro ya kale iliyoishi kwa zaidi ya miaka 1500 hadi 50,000.


Watumishi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar na wengine, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lusius Mwenda (wa pili kulia) katika picha ya pamoja walipotembelea michoro ya miambani Kondoa Irangi, Dodoma. (Picha na Peter Haule, WFM, Dodoma)

 

 Na Peter Haule, WFM, Dodoma

 

Watanzania wametakiwa kuwa na utamaduni wa kutembelea maeneo yenye hadhi ya urithi wa Dunia ikiwemo michoro ya miambani ya Irangi Kondoa Mkoani Dodoma ili kujua historia ya nchi na Serikali inavyohifadhi mali kale kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.

Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lusius Mwenda, wakati wa ziara ya utalii wa ndani wa watumishi 40 wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Zanzibar katika michoro ya miambani Irangi Kondoa Mkoani Dodoma.

Bw. Mwenda alisema lengo la ziara hiyo ni watumishi  waliotoka Zanzibar pamoja na mambo mengine ni kujua fursa za utalii zilizopo Tanzania Bara na kuwa mabalozi kwa wengine wa mali kale adimu nchini.

Kwa upande wake Muhifadhi na Mkuu wa Kituo cha Michoro ya Kondoa Irangi, Bw. Zuberi Mabie, alisema kuwa michoro ya miambani iliyopo Irangi Kondoa ni miongoni mwa hifadhi za mali kale zilizoingizwa katika hadhi ya urithi wa Dunia  mwaka 2006 chini ya Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni  (UNESCO).

Alisema maeneo hayo ya mali kale yana manufaa makubwa kiuchumi kwa kuwa yanatoa fursa za ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambayo mapato hayo yanaenda pia kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.

Bw. Mabie, amewapongeza watumishi hao kutoka Zanzibar kwa kuona umuhimu wa kutembelea michoro hiyo na kujionea jitihada za Serikali za kuihifadhi  na kuwataka watumishi hao kuwa sehemu ya kuhifadhi maeneo hayo muhimu.

Naye Mtumishi wa Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar Bi. Saada Said Seif, alishukuru kwa kupata fursa ya kuona michoro hiyo ambayo alikiri imemvutia na kuwaomba wananchi wengine hususani kutoka Zanzibar wafanye utalii wa ndani wa kwenda kuangalia michoro hiyo.

Michoro ya miambani Kondoa yenye rangi nyeupe, nyekundu na nyeusi  inasadikiwa kuchorwa na Wawindaji na waokota matunda  hasa wa kabila la Wasandawe miaka  1500 mpaka 50,000 iliyopita huku michoro ya rangi nyekundu ikidhaniwa kuwa ya muda mrefu zaidi.

Maeneo mengine yaliyoingizwa kwenye urithi wa Dunia chini ya UNESCO ni pamoja na Mji Mkongwe wa Zanzibar, hifadhi ya Serengeti, hifadhi ya mlima Kilimanjaro, magofu ya Kilwa na Songo mnara na pori la akiba la Selous.

No comments:

Post a Comment

Pages