HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 02, 2022

Waziri Bashungwa:Utekelezaji operesheni anuani za makazi imefikia asilimia 67

Operesheni anwani za makazi sasa ni Asalimia 67

 

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akizungumza wakati wa mkutano na Wakuu wa Mikoa uliofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi.

Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa, John Mongella ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wakati wa mkutano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa lengo la kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa operesheni ya Anwani za Makazi.
 


Na Jasmine Shamwepu, Dodoma



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMO), Innocent Bashungwa amesema kazi ya utekelezaji operesheni ya anuani za makazi kwenye mikoa yote Tanzania Bara imefikia asilimia 67 ya utekelezaji wake.


Waziri Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma leo wakati wa kikao kazi kati ya Wakuu wa Mikoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kuhusu uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa operesheni ya anuani za makazi nchini.


“Tumefikia asilimia 67, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya, sina shaka na wakuu wa mikoa, ninaamini hili la operesheni ya anuani za makazi mtafanya vizuri,”amesema Waziri Bashungwa.


Aidha, Waziri Bashungwa amesema, kwa sasa kazi iliyobakia ni kuongeza hamasa kwenye kazi hiyo na kutoa elimu kwa wananchi ili kazi hiyo iendelee vizuri na kufikia malengo yanayotarajiwa na Serikali.


“Nisisitize kuwa asilimia 67 zilizofikiwa ni hatua nzuri lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya, sina shaka na Wakuu wa Mikoa, ujenzi wa madarasa ya mama Samia mlifanya vizuri hivyo naamini na hili operesheni ya Anwani za Makazi mtafanya vizuri”, Amezungumza Bashungwa


Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema, zoezi la utekelezaji wa operesheni ya anuani za makazi limekwenda vizuri na linatarajiwa kukamilika kabla ya muda uliopangwa ambao ni Mei 22, 2022 ikiwa ni pamoja na kukamilisha mfumo wenyewe wa anuani za makazi ambao upo chini ya wizara yake.


 Nape amesema, kwa sasa Serikali inaendelea kutambua maoni yaliyotolewa, kutoa elimu kwa wananchi, kuandaa taarifa, kutengeneza taarifa hizo na kuziingiza kwenye mfumo ikiwa ni pamoja kuuweka mfumo wenyewe ili ufanye kazi.


Tathimini iliyofanyika ya kupata asilimia 67 imezingatia kazi zilizotekelezwa ikiwa ni kazi ya kutambua maeneo; kujenga uwezo kwa maafisa na watendaji wanaofanya kazi hii; kutoa elimu ya zoezi husika; kukusanya taarifa; kutengeneza mfumo utakaopokea taarifa na kuingiza taarifa kwenye mfumo ili ziweze kutumika na kuweka muundombinu (physical) katika maeneo mbalimbali nchini”, amezungumza Mhe. Nape

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof.Riziki Shemdoe amesema, lengo la kikao kazi ni kujadili namna ambavyo wakuu wa mikoa wanaendelea kutekeleza operesheni ya anuani za makazi Tanzania Bara na kuwa kazi hiyo inakwenda sambamba na Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwezi Agosti, 2022.


Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema zoezi la anuani za makazi linaendelea vizuri kama ambavyo wizara iliwapa maelekezo kwani fedha za kazi hiyo zilipokelewa ijapokuwa kuna maeneo machache ambayo yalikuwa na tatizo la kimtandao wakati wa kutumia fedha za kazi hiyo.


Amesema, baadhi ya changamoto zilijitokeza ni wingi wa watu kwa baadhi ya mikoa pamoja na maeneo makubwa ya makazi, lakini wanashukuru wizara zilituma timu za wataalam katika kusaidia utekelezaji wa kazi hiyo.


Zoezi la anuani za makazi linafanywa na wizara mbili kwa pamoja ambazo ni Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ambalo linatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 22,mwaka huu kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akilizindua mnamo Februari 8, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages