HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 23, 2022

Sheria ya Mtandaoni, hatari iliyojificha: Wakili Marenga


Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN),
James Marenga, akitoa mada katika semina ya waandishi wa Habari za mtandanoni jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akitoa mada katika semina ya waandishi wa Habari za mtandanoni jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu

 

 SHERIA ya Uhalifu wa Mtandaoni iliyotungwa Mwaka 2015, imebeba maneno ambayo, kama utaisoma juu juu unaweza usijue hatari yake.

 

Kauli hiyo imetolewa na James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN) katika semina na waandishi wa Habari za mtandanoni jijini Dar es Salaam.

 

Marenga ambaye ni wakili wa kujitegemea amesema “tusipokuwa makini, sheria hizi zitaumiza wengi.”

 

Wakili Marenga amesema, kwa ujumla wake sheria hiyo imeweka baadhi ya maneno ambayo yanaweza kutumiwa vibaya na mahakama huku tafsiri ya maneno hayo ikiwa imefichwa.

 

Ametaja baadhi ya maneno yenye mitego katika sheria hiyo ikiwa ni pamoja na ‘kwa namna nyingine’ ama ‘kusudio na kinyume cha sheria.’

 

“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria. Maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amesema Wakili Marenga.

 

Kwenye semina na wanahabari hao, Wakili Marenga amesema, kwenye sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Pia amesema, sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.

 

“Sheria hii katika Kifungu cha 50 (2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo. 

 

“Hukumu ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa mahakani lini, na kwa kosa gani. Ndio maana tunasema sheria hii inatakiwa kupitiwa upya,” amesema Wakili Marenga.   

No comments:

Post a Comment

Pages