HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 18, 2022

Mpango Mkuu wa Maji waja Zanzibar

Mkurugenzi wa GWP Dkt Victor Kongo ( kushoto) akitiliana saini ya makubaliano ya Mpango Mkuu wa Maji Zanzibar na Katibu WMNM Joseph Kilangi ( kulia).


Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) imetiliana saini ya makubaliyano (MoU)  na taasisi ya Global Water Partnership (GWP)  kuhusu utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maji safi na Salama  Zanzibar.

 Hafla hiyo ya kutiliana saini imefanyika WMNM Maisara, Zanzibar baina ya Katibu Mkuu Joseph Kilangi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya GWP Dr. Victor Kongo na  kushuhudiwa na Viongozi Wakuu na watendaji wa taasisi mbili hizo.            

Akizungumza Katibu Mkuu WMNM Joseph Kilangi alisema kupitia makubaliyano hayo Mpango Mkuu wa Maji Zanzibar 2022- 2027 utaweza kutekelezeka kwa haraka na kuleta ufanisi ambao Wizara yake inahitaji katika utekelezaji wa huduma ya maji  Zanzibar .

Alisema  changamoto ziliyopo katika masuala ya maji yanahitaji utafiti wa kina ikiwemo miundombinu ya maji, eneo/maeneo sahihi ya kuchimba visima na mambo mengine ya kitalaamu ili Wizara yake iweze  kutatua tatizo la maji  kwa wananchi.

“Taasisi ya Global Water Partnership itaweza kusaidia kufanya tafiti zinazohitajika ili tatizo la maji lipatiwe ufumbuzi kwani maeneo mengi yamekuwa yakikosekana maji kupitia mkutano huu tafiti za kitalamu zitafanywa “ Alisema Kilangi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa GWP Dr. Victor Kongo alisema makubaliyano hayo yataleta ufanisi katika kutekeleza Mpango Mkuu wa maji Zanzibar ambapo Taasisi yake imepanga kufanya tafiti mbali mbali pamoja na kutafuta miradi ya maji kwa Zanzibar.

Alisema kupitia Mkataba huo wa  makubaliano waliyosaini Agosti 17, 2022 Taasisi yake itaongeza juhudi za makusudi ili tatizo la maji Zanzibar lipatiwe ufumbuzi na maji yapatikane katika maeneo yote ya mjini na vijijini.

Kwa upande wake Waziri wa Maji, Nishati Na Madini Shaibu Kaduara alisema wananchi wengi Zanzibar wamekua wakilalamikia masuala ya maji, lakini kupitia tafiti zitakazofanywa baina ya Wizara yake kwa kushirikiana na GWP anaamini Wizara yake itafanikisha kuwaondolea shida ya maji katika mji wa Zanzibar.

Kwa upande wake mwenyekiti wa GWP mhandisi Ngwisa Mpembe ameahidi kuleta watalaamu wa utafiti katika masuala ya maji Zanzibar hivyo ameiomba Wizara ya Maji, Nishati na Madini kuingiza masuala ya utafiti katika Mpango Mkuu wa Serikali.

Mwisho alimshukuru  Waziri wa Maji , Nishati na Madini Shaib Kaduara, Katibu Mkuu Joseph Kilangi bila ya kumsahau Katibu Mkuu aliyeondoka Dkt Mngereza Miraji kwa kuwapokea na kuanzisha mashirikiano ya pamoja kwa ajili ya kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi huduma ya Maji Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

Pages