HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 20, 2022

Z'BAR SENSA MARATHON KUTIKISA


Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mashindano ya Zanzibar Sensa Marathon, Catherine Peter Nao akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa idara ya habari maelezo Zanzibar juu ya maandalizi ya Zanzibar Sensa Marathon.

 

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR

 

Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya mashindano ya Zanzibar Sensa Marathon, Catherine Peter Nao, amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mashindano hayo.

Alisema mashindano hayo licha ya kuwa sehemu ya kuhamasisha sensa bado yana faida za kipekee za kuweka sawa utimamu wa mwili kwa kufanya mazoezi ya viungo na kudumisha michezo nchini.

Hayo ameyaeleza leo wakati akizungumzana na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara maelezo Zanzibar, alisema katika kuhakikisha kila mtu anashiriki kutakuwa na vituo vitatu vitakavyofunguliwa kwa ajili ya kutoa fomu za ushiriki.

Alisema fomu za mashindano hayo zinatarajiwa kuanza kutolewa Agosti 17 hadi 19 mwaka huu.  

Catherine alifafanua kuwa utaratibu wa uandikishwaji wa washiriki utafanyika kuanzia tarehe 17 Agosti hadi 19 mwaka huu 2022 katika ofisi za Chama cha Riadha Zanzibar iliopo Amani uwanjani,Ofisi za Bahari Fm na viwanja vya Kisonge kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 10 jioni.

Mwenyekiti huyo alisema mashindano hayo ya Zanzibar Sensa Marathon ya umbali wa kilomita 10 yatafanyika siku ya Jumamosi ya Agosti 20 mwaka huu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla. 

Alisema ili kufikia azma ya serikali zote mbili ya kufanikisha zoezi hilo kupitia vituo vya Uhuru Fm na Bahari Fm kwa kushirikiana imeandaa mashindano hayo ikiwa na lengo la kuhamasisha watu kujitokeza kwa wingi siku hiyo.

"Pia ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa watakaopita majumbani mwao na kutoa taarifa muhimu na kwa usahihi ili kuiwezesha serikali kupata takwimu sahihi zitakazo wezesha kupanga kwa usahihi maendeleo ya watu,"alisema

Alisema pia mashindano hayo yatahusisha pia watu wenye ulemavu ambao watakimbia umbali wa kilomita 3 na kwamba matarajiao ya kamati watajitokeza kwa wingi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Riadha kutoka Chama Cha Riadha Zanzibar, Masoud Tawakal Khairailla alisema mashindano hayo ya Zanzibar Sensa Marathon yatakuwa ni ya umbali wa kilomita 10.

Alisema mashindano hayo yataanza katika eneo la Kisonge kupitia njia ya Madema hadi Maisara na kuelekea Kilimani,Migombani hadi Mazizini kupinda njia ya ZRB hadi aroundi about ya Mombasa na kupitia SOS.

"Pia watapita Shimoni,kwa mchina mata na kupinda kupitia njia ya Jangombe hadi Mzizima na kupita Barabara ya Mlimau,kwa Chimbeni,matarumbeta na kupida kupitia kibanda hatari,kwa Muhamed Ali,Kwahani,kwaalinatu hadi Kariakoo na kupinda kuelekea Kachorora hadi Mapinduzi Square Michenzani,"alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages