HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2022

Profesa Mkenda azindua mradi wa HEET, awaonya wakuu wa vyuo

 

 

Na Irene Mark

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewataka wakuu wa vyuo vya umma kuwaruhusu wahadhiri wa vyuo vyao kwenda masomoni badala ya kuwawekea vikwazo na kutumia vibaya madaraka yao.

Waziri Mkenda amesema hayo leo Septemba 13,2022 alipokuwa akizindua Mradi wa miaka mitano wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET Project), jijini Dar es Salaam na kuwataka wakuu wa vitengo, idara na vyuo kutumia madaraka yao vema.

Mradi wa HEET wenye thamani ya sh. Bilioni 972 ambazo ni mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia zitatumika katika utekelezaji wa mradi huo kwa miaka mitano hapa nchini umedhamiria kuboresha elimu kuanzia ngazi za msingi hadi vyuo vikuu.


Maeneo yatakayoguswa kwenye mradi huo ni ujenzi wa vyuo vikuu vya umma na kampasi zake kwenye mikoa mbalimbali, kuwaendeleza kielimu wahadhiri, kuboresha stadi za ufundishaji kwa njia ya TEHAMA na kuhakikisha ujuzi unapatikana kwa wanafunzi.

Amesema mradi huo utasomesha wahadhiri wa vyuo vya umma na binafsi kwa sekta ya afya na tiba ndani na nje ya nchi kwa fani mbalimbali.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa uwazi na bila upendeleo hivyo kila mhadhiri atakayekidhi vigezo atapata fursa ya kuongeza elimu yake kwa ngazi anayostahili.

“Dunia nzima inazungumzia elimu. Mradi huu umedhamiria kuboresha elimu yetu na hakuna atakayeachwa nyuma... Dola milioni 1.1 za Marekani zimetengwa katika mradi huu kwa ajili ya kuwaendeleza kielimu wahadhiri wa vyuo vikuu binafsi kwa sekta ya tiba na afya.

“Namna tunavyoendesha elimu yetu kwa level ya vyuo vikuu inaakisi ubora wa elimu tunayoitoa kwa ngazi za chini, sasa HEET inatupa push katika elimu kuanzia miundombinu, majengo na ubora wa watoa elimu wenyewe,” amesema Profesa Mkenda.

Katika uzinduzi huo Profesa Mkenda aliwapa vyeti wahadhiri 11 kutoka vyuo vikuu mbalimbali wanaokwenda nje ya Tanzania kuongeza elimu na ujuzi kwa sekta tofauti.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Francis Michael amesema mradi wa HEET utawanufaisha wahadhiri 1,100 kwa kuwaongezea ujuzi na elimu kwa sekta walizopo.

Dk. Michael aliwasisitiza wasimamizi wa mradi huo kutoa fedha za mradi kwa mujibu wa maelekezo na sio vinginevyo.

“Kila fedha ya mradi itatumika kama ilivyoelekezwa nawasihi sana wasimamizi wa mradi huu, pakitokea changamoto au mkwamo kwenye fedha hizi ofisi ya Katibu Mkuu ipo wazi njoo tujadiliane msizitumie vibaya hizo fedha tafadhali,” amesisitiza Dk. Michael.

Utekelezi wa mradi wa HEET utanufaisha vyuo 14 vya elimu ya juu na taasisi 5 zinazoshughulikia elimu.

Uzinduzi wa mradi huo ulihudhuriwa pia na wakuu mbalimbali wa vyuo vikuu na wahadhiri, mwakilishi wa Benki ya Dunia, wadau wa sekta ya elimu na wakuu wa taasisi za kielimu zinazonufaika na mradi huo.

No comments:

Post a Comment

Pages