NA CHRISTINA MWAKANGALE
NI
ndoto ya kila mwanamke kwamba afikapo umri wa utu uzima iwe ameolewa au
hajaolewa, kupata mtoto, ingawa matarajio hayo kwa wenye imani tofauti
ikiwamo dini ni kudra za mwenyezi Mungu.
Pamoja
na matarajio hayo, ugumba hukatiza ndoto za wanawake wengi. Ugumba ni
tatizo la kushindwa kushika mimba kwa njia ya kibaolojia na linatibika.
Kadhalika
mabingwa wa kinamama na uzazi, watatafsiri ugumba ni hali ya mwanamke
kushindwa kupata ujauzito kwa kipindi cha mwaka mmoja, ilhali upo kwenye
ndoa au mahusiano na hatumii njia yeyote kuzuia mimba.
Pamoja
na hayo, kukua kwa teknolojia duniani kumetafsiri tofauti hali hiyo, na
kurudisha faraja kwa wanawake waliosubiri ujauzito muda mrefu, kwa njia
ya kiteknolojia, ikiwamo huduma ya kupandikiza mimba (In vitro
Fertilization-IVF).
Veneranda
Alfred (48), anajihisi ndoto hiyo haijatimia kwake hadi sasa, licha ya
kuwashirikisha viongozi wa dini wa kanisa anakosali ya kile kinachomsibu
kwa muda mrefu, akiwataka wamfanyie maombi, apate mtoto.
Anasema
ametarajia kupata mtoto kwa takribani miaka 10 bila mafaniko, akiuona
umri ukimtupa mkono na hajafanikiwa kuitwa mama na kuamua kutumia fedha
yake kwa kiwango chochote kugharamia IVF.
IVF
ni mbinu ya kisasa ya kitabibu inayowezesha mfumo wa kuunda mimba
kiteknolojia hospitalini, ambayo imekuwa maarufu, nchi za Afrika ikiwamo
Tanzania, huku watoto milioni nane wakikadiriwa kuzaliwa kutokana na
IVF, kwa mujibu wa European Society of Human Reproduction and
Embryology.
Bingwa wa
Magonjwa ya Wanawake na Uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Dk. Living Colman, anasema kesi za wenza kushindwa kupata watoto
zinaongezeka na kwamba kwenye kliniki kati ya wagonjwa 10 ambao anawaona
kila siku hospitalini hapo, watatu wana tatizo hilo, ambalo kitaalamu
anataja ni ugumba (infertility).
Kwa
takwimu hizo za mtaalamu huyo kutoka MNH, ni kwamba wenye tatizo la
ugumba kwa mwezi kutokana na idadi hiyo, huonwa watu 90 na kwa mwaka
ikifikia 1,080 wanaohitaji kutibu ugumba.
SIMULIZI YA VENERANDA
Veneranda
ni mkazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam, ni mjasiriamali ambaye mara
baada ya kufanya shughuli zake, muda wa jioni kwa siku tatu za wiki,
huutumia kwa kushiriki na waumini wenzake, kanisani kwa ajili ya kusali
na shughuli zingine.
Anasali
kanisa ambalo halipo mbali sana kutoka nyumbani kwake anakoishi, na
ameishi Tabata kwa takribani miaka 20 na ameweza kujenga nyumba yake.
“Ninaishi
pekee yangu, sina watoto, mara chache au siku za likizo watoto wa ndugu
zangu huja kunitembelea au watoto wa marafiki zangu ambao ninasali nao
kanisa moja. Kuna wakati huwa najihisi mpweke, nina bahati mbaya.
Wenzangu ambao nina umri au Rika moja, ama nimesoma nao hasa wanawake,
wana watoto. Jamii inakutafsiri tofauti, dini nako mtihani,” anasema na
kuongeza:
“Kuna wakati
siku tulipotoka kwenye ibada ya Jumapili, mmoja wa muumini mwenzangu,
mwanaye mwenye umri kama wa miaka nane, tisa, alimuuliza mama yake swali
ambalo nilijihisi vibaya, alimwambia...mama tunataenda kwa aunt
Veneranda, amesema niende. Mama yake akamjibu utacheza na nani,
utamsumbua aunt, mtoto wake akamjibu mama yake…nitacheza na watoto wake!’
Veneranda
anasema jibu la mwisho lilimfanya ajisikie vibaya, kisha mazungumzo
hayo yalikatishwa baada ya mama wa mtoto kuamua kumuondoa mwanaye
kisaikolojia, akimwambia akajumuike na watoto wenzie kucheza, na aache
maswali mengi.
“Kwa imani
ninakoabudu nafahamu ninachokwenda kukiamua kitanigharimu, kanisa letu
kupata mtoto ni majaliwa ya Mungu, na muumini yeyote hutakiwi kutumia
njia yeyote mbadala na ukibainika unaweza kuitwa na viongozi wa kanisa
au kutengwa. Hivi sasa nimeanza kufanyiwa vipimo na moja ya hospitali
binafsi, ili nipandikize mtoto kwa IVF,” anasema Veneranda na kuongeza:
“Na
mwanzo wa huduma hii ninatakiwa kukaa ‘bed rest’ (mapumziko) nisifanye
kazi ngumu. Kanisani sijaonekana takribani miezi miwili na sijamtaarifu
kiongozi yeyote, watakapofahamu, sijui itakuwaje.”
TATIZO LILIKO
Bingwa
wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, (MNH), Dk. Colman anasema ugumba ni
hali ya mume na mke, kushindwa kupata ujauzito kwa zaidi ya mwaka mmoja,
bila ya kutumia uzazi wa mpango wowote.
“Mzizi
wa 'infertility' inategemea na chanzo, kwa mwanamke chanzo kikuu ni
hormonal cimbalance' (mayai kushindwa kupevuka kwa mpangilio) na hii
inaweza kutokana na ‘genetics’ (urithi) lakini pia ulaji mbaya, sukari
nyingi na mafuta, husababisha unene uliopitiliza.
“Pia
kupungua sana uzito (anorexia nervosa) inaweza kusababisha ugumba.
Mirija kuziba ndio sababu ya pili ya ugumba kwa mwanamke na hii
husababishwa na ngono zembe kama nilivyoeleza.
Anasema
kwamba, kwa mwanaume sababu ya ugumba inaweza kutokana na kushindwa
kuzalisha mbegu, kutokana na mambo mbalimbali, ikiwamo ulevi wa
kupindukia, sigara na pia kuziba kwa virija vya kupitisha mbegu
inayosababishwa na maambukizi kama ya PID.
“Tiba
ya ugumba ni kumuona mtaalamu wa afya (gynecologist) ambapo atafanya
vipimo na kugundua tatizo halafu atatoa tiba husika. Kama ni ‘hormonal
imbalance’ atapewa dawa na ushauri. Kama mirija imeziba atashauriwa
apandikize (IVF).
“Si
kweli kwamba matumizi ya dawa za uzazi wa mpango ndio chanzo cha ugumba.
Ikiwa zitatumika kwa maelekezo ya mtaalamu, husaidia kuzuia mimba kwa
muda fulani.
“Kuwapa
watoto dawa za uzazi wa mpango ni kuwapa uhuru wa kufanya ngono zembe,
hali inayosabisha kupata maambukizi kwenye via vya uzazi (PID) hivyo
kuathiri mirija ya uzazi na kushindwa kupata ujauzito.
Bingwa
huyo wa kinamama, anasema kwenye jamii hasa mijini wengi wanatumia njia
uzazi wa mpango wa dharura (emergency contraceptive pills) maarufu P2
akiitaja njia hiyo si sahihi kwa kuwa, ikitumika mara kwa mara inapoteza
maana yake.
Bingwa huyo
anashauri kwamba, watoto wafundishwe kuepuka ngono za utotoni, ambazo
ndio chanzo cha maambukizi kwenye via vya uzazi (PID) na kusababisha
kuziba mirija na kushindwa kupata mimba.
HUDUMA YA IVF
Huduma
ya IVF, ambayo mahitaji yanaongezeka, tayari MHN imeanza maandalizi na
maboresho ya kituo rasmi kwa ajili ya huduma hiyo hospitalini hapo
ikiwamo ununuzi wa vifaa.
Mkuu
wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Aligaesha akizungumza
hivi karibuni, anasema maandalizi ya utoaji huduma ya IVF yanaendelea
hospitalini hapo na kwamba yatakapokamilika taarifa itatolewa kwa umma.
Bingwa
na Mtaalamu wa kutengeneza Watoto kwa njia ya teknolojia (Embriologist)
kutoka Hospitali ya Kairuki Green IVF, George Tryphone, anasema
hospitali hiyo imeanza kutoa huduma ya upandikizaji baada ya kubaini
mahitaji ni makubwa, na tayari kwa mwaka huu awamu ya kwanza
wamehudumiwa wanawake 10 na saba ni wajawazito.
Anasema
kati ya hao saba, mmoja ana umri wa miaka 52 sasa ni mjamzito, na
kwamba gharama za huduma ya IVF huwa ni kati ya shilingi milioni 10 hadi
17 kutegemeana na ukubwa wa tatizo.
SIKU YA UGUMBA DUNIANI
Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Merck Foundation, Seneta Dk. Rasha Kelej,
akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari kutoka barani Afrika,
ikiwamo Tanzania, kwa njia ya mtandao, kuadhimisha mwezi wa kujenga
uelewa kuhusu ugumba duniani (World Infertility Awareness Month),
anasema asilimia 50 ya tatizo la ugumba, huchangiwa na pande zote mbili.
Anasema
mwezi Juni, kila mwaka ni maalumu kwa ajili ya kutoa elimu kwa jamii
kuhusu tatizo hilo, ili kuondoa unyanyapaa miongozi mwa jamii, akisema
wanawake ambao hukosa watoto na wamo kwenye ndoa, hunyanyaswa na
kunyanyapaliwa zaidi na ndugu upande wa mume, hasa mawifi, shemeji na
wakwe.
“Tatizo la ugumba
hasa Afrika matokeo ya utafaiti yamebaini kwamba asilimia 75
yanachangiwa na tiba isiyo sahihi kwa walioambukizwa magonjwa
mbalimbali. Mradi wa ‘More Than a Mother and More Than a Father
campaign’ unakuja kutoa elimu na kuondoa unyanyapaa,” anasema Dk. Rasha.
Profesa
Uldapo Ashiru, Rais wa Jumuiya ya Kiafrika inayoshughulikia masuala ya
Uzazi (African Reproductive Care Society-ARCS), kutoka nchini Nigeria,
anasema ugumba limekuwa tatizo la kidunia, huku takwimu za tatizo hilo
zaidi likiongezeka kwenye nchi za Afrika, akitaja sababu mojawapo ni
msongo wa mawazo.
“Nimefanya
kazi kwa miaka takribani 42, zamani wakinamama walifika kliniki peke
yao kuhusu tatizo hili, lakini sasa hata wanaume wana tatizo. Mwanamke
akifikisha umri wa miaka 37 na kuendelea vikwazo vya kutopata ujauzito
huongezeka. Sasa Nigeria kuna mfumo ambao unamwezesha mwanamke kutunza
mayai yake kwenye benki maalum kama ilivyo benki ya damu.
“Mayai
hutunzwa kwa muda mrefu, teknolojia hii inasaidia wanawake ambao kwa
sasa hawapo tayari kupata mtoto kutokana na shughuli za masomo, kazi au
kuchelewa kuolewa. Atakapofikisha umri wowote akishindwa kupata ujauzito
atapandikizwa mayai aliyoyatunza benki, hata akiwa na umri wa miaka
50,” anasema bingwa huyo wa kinamama na uzazi.
Rais
wa Shirikisho la Muungano wa Vyama vya Uzazi (International Federation
Fertility Societies and Gynaecologist), Dk. Edgar Macanu anasema tatizo
la ugumba, linajitokeza zaidi kwa wanawake kuanzia umri wa miaka 37 na
kuendelea, kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo za kimazingira au
kibaolojia.
No comments:
Post a Comment