HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 12, 2023

DKT. NDUMBARO AELEZA MAFANIKIO LUKUKI YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA MIAKA MITANO SONGEA MJINI

 


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho kushoto akizungumza jambo na Mbunge wa Songea Mjini Dkt Ndumbaro wakati wa Mkutano Mkuu wa Jimbo hilo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini James Mgego akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo.

 

NA STEPHANO MANGO, SONGEA

 

VIONGOZI wa Chama cha Mapinduzi Mkoani Ruvuma wametakiwa kuyasema mazuri yote yanayofanywa na Rais, Wabunge na Madiwani ili wananchi waelewe kwa uwazi mambo hayo ambayo kimsingi yameainishwa kwenye ilani ya CCM ya mwaka 2020/ 2025.

Hayo yameelezwa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo la Songea Mjini wa kupokea Utekelezaji wa Ilani ya CCM Katika Kipindi Cha Miaka mitano tangu 2018 - 2023 ya Uongozi wa Dkt.Damas Ndumbaro Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini na Waziri Wa Katiba na Sheria, Ulioifanya Songea Mjini.

Mwisho alisema kuwa yapo ambayo yamefanyika na yanaonekana kwenye sekta mbalimbali lakini viongozi wa Ccm kwenye maeneo yenu hamyatangazi, hali ambayo inapelekea kuzuka kwa masikitiko kwa wananchi

Leo Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Ndumbaro ameyaeleza mafanikio aliyoyapata kwa miaka mitano toka 2018-2023 na ameyaandika kwenye kitabu chenye kurasa 140, myasome na myaeleze waziwazi ili wanachama na wananchi wayaelewe namna Mbunge anavyohangaika kuwaletea maendeleo

“Nakupongeza sana Mbunge Dkt Ndumbaro kwa kazi kubwa unayoifanya katika Jimbo lako na Nchi kwa ujumla, sie kama chama ndio tulikukabidhi Ilani ili uitekeleza hakika umefanya makubwa kwa muda mfupi, hongera sana na tutaendelea kuyasema haya kila mara ili kukirahisishia chama katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na vijiji mwaka 2024 na uchaguzi mkuuu mwaka 2020” alisema Mwisho

Akisoma ilani hiyo ya miaka mitano Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dkt Damas Ndumbaro ambaye pia ni Waziri wa Sheria na Katiba alisema kuwa mambo mengi yametekelezwa katika sekta zote na kuwafanya wananchi waendelee kufurahia uwepo wa Viongozi wanaotokana na Ccm

Dkt Ndumbaro alisema katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2023 Serikali imetekeleza na kuendeleza  miradi mbalimbali ikiwemo na ujenzi wa vyumba vya madarasa fedha za UVIKO 19, ujenzi wa vituo vya afya vipya  vitano 5 na Hospitali ya Wilaya 1 pamoja na Hosptali ya Rufaa ya Mkoa  1 iliyopo Mwengemshindo,

“Kujengwa Chuo kikuu kipya cha Uhasibu Arusha, Masoko mawili ya kisasa (Manzese), ujenzi wa uwanja wa ndege, daraja  ya Matarawe- Mjiwema, Mikopo kwa vikundi bil. 1 kwa mwaka, Barabara kutoka Sanga one hadi Tanroad, kujenga barabara ya kiwango cha Lami km 13 katika kata ya Mfaranyaki, Misufini, na  Majengo na miradi mingineyo kutawafanya wananchi kupiga hatua ya kimaendeleo” alisema Dkt Ndumbaro.

Alisema pamoja na ukarabati wa  miundombinu chakavu  ya madarasa, barabara za mitaa, maji kwa baadhi ya kata, uhitaji wa vituo vya afya katika kata ya Bombambili, Ruhuwiko, na Lizaboni, uhitaji wa shule za Sekondari mpya kwa kata ambazo hazina Sekondari za kata kama Seedfarm, Ruhuwiko na Ndilima Litembo.

Naye Mstahiki Meya Manispaa ya Songea Michael Mbano  amesema Manispaa imetenga bajeti ya shilingi Mil. 20 kupeleka kila kata ambazo zitasaidia kutatua changamoto  mbalimbali za kata husika ikiwemo ukarabati wa miundombinu ya madarasa chakavu.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Dkt, Frederick Sagamiko alisema changamoto ya barabara za mitaa haita kuwepo kwa sasa kwani Manispaa imeandaa utaratibu kupitia TARURA wa kutatua chanagamoto hizo ambapo ameagiza kata zote 21 kuleta taarifa zenye ufafanuzi maalum wa mahitaji ya miundombinu  korofi ambayo inahitaji kutekelezwa ikiwemo na  barabara za mitaa, vivuko vyote, madaraja, na mifereji ili TARURA waweze kutekeleza .

Mwenyekiti wa CCM Wilaya Songea Mjini Mwinyi Msolomi amewataka Viongozi mbalimbali kuacha Mipasuko ambayo itapelekea  kuzorotesha  shughuli za kimaendeleo.

Msolomi alisema lengo kuu la Serikali katika kuaajiri wataalamu ni kwa ajili ya kusimamia na kuratibu  shughuli shughuli zote za  Serikali pamoja na kusogeza huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake Katibu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini James Mgego  alisema kuwa Wananchi wa Songea  wana kila sababu ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ikiwemo kutoa fedha nyingi ambazo zimekwenda kutekeleza miradi mbalimbali

Mgego alisema katika kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2022/2023  Halmashauri ya Manispaa ya Songea imepokea fedha kiasi cha Tshs. 750,000,000.00 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya Manispaa, Zahanati ya Makambi na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitenganishi kwaajili ya vituo vya kutolea huduma za dawa.

No comments:

Post a Comment

Pages