*Sombi aahirisha mwaliko wa Kenya
NA TULLO CHAMBO, RT
TIMU ya Taifa ya Tanzania ya Mbio za Nyika 'Cross Country', imeanza kambi kujiwinda na Mashindano ya Dunia yanayotarajiwa kufanyika nchini Australia, Februari 18 mwaka huu.
Timu hiyo chini ya jopo la Makocha linaloongozwa na Denis Male, imeanza kambi Februari Mosi katika Hoteli ya Mbono, Ngaramtoni jijini Arusha.
Wachezaji wanaounda timu hiyo ni Josephat Gisemo, Inyasi Sulle, Fabiano Nelson na Mathayo Sombi, huku ikitarajiwa kuondoka nchini Februari 14, kuelekea nchini Australia kwa ajili ya mashindano hayo.
Akizungumzia mazingira ya kambi, Kocha Male, alisema ni mazuri na kwamba kwa ushirikiano, atahakikisha wanawajenga wachezaji kisaikolojia na kihamasa ili kuhakikisha wanakwenda kulipambania vema Taifa.
Katika hatua nyingine, mchezaji Mathayo Sombi, ambaye alikuwa amepata mwaliko kwenda kushiriki Cross Country nchini Kenya, sasa hatakwenda kutokana na sababu za kiufundi.
Makocha pamoja na mchezaji huyo, wamekubaliana ajikite na kambi ya Taifa, kwani muda uliosalia kwa mashindano ya Dunia ni mfupi.
No comments:
Post a Comment