HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 02, 2023

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YALAANI VIKALI ONGEZEKO WANANCHI KUVAMIA, KUJERUHI NA KUUA ASKARI NA WATUMISHI WA UHIFADHI

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alipokuwa akijibu hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii katika Bunge la Kumi na mbili leo Jijini Dodoma.

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Wizara ya Maliasili na Utalii imelaani vikali kufuatia matukio ya Askari wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu  kuvamiwa na kuuawa na wananchi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao kisheria.

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana ametoa kauli hiyo   leo Jumatano  Februari 2, 2022 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akijibu hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii

 

Amesema kuanzia Machi mwaka jana hadi Februari mwaka huu  jumla ya askari wa Uhifadhi na Watumishi 9 wameuawa huku jumla ya  Askari wa Uhifadhi na Watumishi 68  wamejeruhiwa.  

 

Amesema baadhi ya wananchi wanapokamatwa kwa makosa ya kuingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria kumekuwa na tabia ya wananchi kujipanga na kuvamia askari au kambi zao na kuwashambulia kwa silaha mbalimbali za jadi kama vile fimbo, sime, mapanga na  mishale

 

Ameongeza kuwa matukio haya yamekuwa yakijrudia mara kwa mara katika maeneo mbalimbali hapa nchini na mara nyingi yamekuwa yakitokea pindi askari wa Jeshi la Uhifadhi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi

 

Amesema matukio haya yamepelekea askari wa Jeshi la Uhifadhi kujeruhiwa au kuuwawa pamoja na kusababisha uharibibifu wa mali za Serikali kama vile kuchoma moto magari, nyumba na vitendea kazi vingine muhimu kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Balozi Dkt. Chana amewataka wananchi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za Wanyamapori na Misitu hapa nchini na kuwataka wale wote wanaojichukulia sheria mkononi waache vitendo hivyo mara moja  kwani ni  kinyume cha sheria za nchi.

 

 Aidha, Amesema Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama ili kukomesha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja na kuwabaini wale wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine ili sheria ichukue mkondo wake.

 

No comments:

Post a Comment

Pages