Na Mwandishi Wetu
Asikwambie Mtu, kazi ni moja tu kwa Wananchi. Kushinda mechi zao zilizobaki hayo mengine hayawahusu. Wanaanza na KMC leo pale pale 'Lupaso' Benjamin Mkapa majira ya saa 16:00 kwa saa za Afrika Mashariki na Kati.
Wanaingia wakihitaji alama tatu muhimu na wakizipata kwao ni furaha bila kujali kilitokea nini Jana kwa wapinzani wao Simba dhidi ya Azam FC kwani watafukisha pointi 62 huku Mnyama akisalia na pointi 54 tofauti ya pointi 8 kila timu ikisaliwa na michezo saba.
KMC licha ya kuwa timu sumbufu hasa inapokutana naYanga lakini bado rekodi bora ya ushindi Iko kwao kwa kushinda mechi nyingi zaidi na KMC wao wakishinda mechi moja tu.
Miamba hiyo ya Dar es Salaam imekutana mara tisa za ligi, Yanga wameibuka na ushindi kwenye mechi sita, ikipoteza moja na kutoka sare michezo miwili, ikifunga mabao 12 huku KMC ikiweka kambani mabao matano tu.
KMC hawako katika mtiririko bora wa kupata matokeo jambo ambalo linawaweka nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu na pointi zao 22 walizokusanya katika michezo 22.
Kuelekea mchezo wa leo Kocha Msaidizi wa KMC Ahmad Ally amesema watapambana kuhakikisha wanafanya vizuri dhidi ya Yanga ili wajiondoe katika nafasi waliyopo sasa.
“Tangu mechi ya mwisho tulipocheza tumepata mechi tatu za kirafiki ambazo zimewajengea wachezaji utimamu wa mwili ingawa sio za kimashindano tofauti na wapinzani wetu ambao walikuwa katika mechi za kiushandani. Wachezaji wetu wapo katika morali kubwa ya mechi ingawa tutamkosa Hance Maoud ambaye ni majeruhi wa muda mrefu,” amesema Ally.
Wakati huo huo Mabingwa watetezi Young Africans wametamba kuchukua alama tatu ili wazidi kujikita katika kilele cha msimamo wa ligi.
“Kikubwa ambacho tumekifanya kwa wachezaji ni kuwakumbusha waachane na furaha ya ushindi katika mchezo uliopita dhidi ya TP Mazembe na akili yao ifikirie zaidi mchezo dhidi ya KMC ambao uko mbele yetu tunaohitaji kupata ushindi ili utuweke katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wetu,” amesema Kocha msaidizi wa Yanga Cedrick Kaze.
No comments:
Post a Comment