HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 22, 2023

TMA, wanahabari kuongeza ushirikiano

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a (aliyesimama), akizungumza na waandishi wa habari wabobevu kwenye sekta ya hali ya hewa wakati wa semina ya siku moja iliyofanyika leo Februari 21,2023 mjini Kibaha, Pwani. Aliyeketi pembeni yake ni Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi na Vifaa vya mamlaka hiyo, Dk. Pascal Waniha.


Na Irene Mark, Kibaha


KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’a, ameahidi kuongeza ushirikiano na vyombo vya habari ili kuendelea kuboresha viwango vya usahihi wa taarifa za mamlaka hiyo kwa jamii.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Mkoa wa Pwani leo Februari 21,2023 wakati wa semina ya siku moja kuhusu utabiri wa msimu wa masika utakaoanza Machi, Aprili na Mei, mwaka huu, Dk. Chang’a alisema viwango vya usahihi wa utabiri wa mvua za vuli zilizoanza Oktoba, Novemba na kumalizika Desemba, 2022 umekuwa bora kwa asilimia 94.1.


Amesema baada ya semina, timu ya wafanyakazi wa TMA itafanyia kazi mapendekezo ya wanahabari waliohudhuria semina hiyo huku wakisisitiza ushirikiano wa pande hizo mbili uhusishe pia wanahabari wanaochipukia kwenye sekta ya hali ya hewa.


“Tumeyachukua maoni na ushauri wenu tunawaahidi kuyafanyiakazi ili kuboresha utendaji wa mamlaka yetu, waandishi wa habari za hali ya hewa na usahihi wa taarifa zetu ambazo ninyi mnatusaidia kuzifikisha kwa jamii.


“Katika kutekeleza maazimio haya, ushauri wenu wa sisi kutembelea vyombo vya habari pengine tutaanza utekelezaji wake haraka zaidi na mtaona matokeo yake,” alisema Dk. Chang’a na kusisitiza kwamba lengo ni kuhakikisha sekta ya hali ya hewa Tanzania inakuwa bora leo kuliko jana na kesho kuliko leo.


Akizungumzia ushirikiano uliopo sasa kati ya mamlaka hiyo na wanahabari, Kaimu Meneja Uhusiano wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Monica Mutoni, alisema wanawaunganisha wanahabari hao na fursa mbalimbali za mikutano, mafunzo na makongamano ndani na nje ya nchi.


Mutoni alisema “Mfano Desemba,2022 tulifanikiwa kuwapeleka waandishi wa habari 10 wabobezi wa taarifa za hali ya hewa kwenye mafunzo jijini Nairobi nchini Kenya ili kushuhudia namna nchi washirika wa kanda yetu hapa Afrika wanavyofanya kwenye kuchakata na kusambaza taarifa za hali ya hewa.


“...Si hivyo tu inapotokea taarifa yenye kuzua taharuki kwenye mitandao ya kijamii mfano kimbunga “Freddy” licha ya kwamba ilikuwa siku ya jumapili wengi wao walinipigia kutaka ukweli wa taarifa ile na usahihi wake.


“Mifano ya ushirikiano ni mingi kwa kweli ambayo imetuunganisha kuwa familia moja inayoshikana mikono na kutembeleana kwenye hali zote, misiba, harusi, maradhi na namna yeyote ya kusaidiana kijamii huwa tunafanya hivyo kwa umoja.”


Akiishukuru timu ya wafanyakazi wa TMA kwa niaba ya waandishi wengine, Dorcas Raymos kutoka kituo cha luninga cha Channel10 alisema chini ya mamlaka hiyo, wamejifunza mengi na kujiona kama sehemu ya wafanyakazi wa mamlaka katika jamii kwa kuwa wanashirikishwa kwenye maandalizi ya utabiri na kupewa taarifa sahihi zinazojitosheleza na kuziwasilisha taarifa hizo kwa jamii kupitia vyombo mbalimbali vya habari wanavyovitumikia.


Hii ni mara ya 22 tangu TMA ianzishe utaratibu wa kuwashirikisha waandishi wa habari na kuwaonesha namna wanavyokusanya taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya kisayansi na kuzichakata kisha kupata utabiri wenye viwango vya usahihi kwa zaidi ya asilimia 90 ikilinganishwa na viwango vya kidunia ambavyo ni asilimia 70.

No comments:

Post a Comment

Pages