NA TULLO CHAMBO, RT
WANARIADHA 19 wamefanikiwa kuchaguliwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 18 na 20 itakayoiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Afrika Mashariki (EAAR U 18 & U 20 yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia Machi 9 mwaka huu.
Wanariadha hao wamepatikana kupitia mashindano ya wazi ya Taifa, yaliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam Machi 4 mwaka huu, ambayo yaliandaliwa na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).
Jopo la Wataalamu wakiongozwa na Makocha wa Taifa wa timu hiyo, Robert Kalyahe na Mwinga Mwanjala Soote, lilichagua wanariadha hao kutokana na viwango ambavyo wanariadha hao walivionyesha na si kutokana na nafasi walizoshika katika mchezo husika.
Aidha makocha hao, walibainisha kuwa wameshuhudia vipaji vipya vingi wameviona na kama vikiendelezwa vitakuja kuwa lulu kwa Taifa siku zijazo.
Kutokana na vijana hao 19 waliofuzu, wengine nane watajumuishwa nao ambao walifanya vema katika mashindano mengineyo ikiwemo Ladies First yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada kutangazwa timu hiyo mbele ya viingozi wa mikoa iliyoshiriki Tabora, Mbeya, Pwani, Dar es Salaam, Arusha, Morogoro, makocha mbalimbali na Waandaaji wa Matukii ya Riadha 'Race Organizers' (RO's), Makamu wa Rais wa RT, William Kallaghe, aliwapongeza wote waliofanikisha tukio hilo na kubainisha kwamba, kati ya malengo makuu ya shirikisho hivi sasa ni kuwekeza kwa vijana ambao ndio hazina ya Taifa.
"Kati ya mikakati mikubwa hivi sasa ya RT ni kwenye mbio za uwanjani....Na hakuna ujanja bali kuwekeza kwa vijana na ndio maana tunawaomba na kuwahimiza wadau kusapoti katika hili.
"Vijana hawa tuliowapata ndo tunaanza nao, hivyo tunawaomba wadau mbalimbali mtuunge mkono katika hili kwa manufaa ya Taifa siku zijazo, na ambao leo hamkufanikiwa kuingia katika timu hii, msikate tamaa kwani bado nafasi mnayo mzidishe juhudi," alisema Kallaghe na kuongeza.
Timu hiyo itaingia kambini mapema Jumatatu kwenye hosteli za Baraza la Maaskofu (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.
Wanariadha 19 waliopenya ni pamoja na Siwema Julias, Shija Donald, Salma Samwel, Christina George, Elizabeth Kirario, Bravo George, Kimena Kibase, Damian Christian, Fedelis Amadi, Baraka Tiluli na Emmanuel Amos.
Wengine ni Elizabeth Ilanda, Gaudensia Maneno, Elia Clement, Nicodemus Joseph, Nelson Mangura, Jackson Sylvester, Dickson Mangura na Malcolm Kazmir.
No comments:
Post a Comment