HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 09, 2023

SAMAF, Jeshi la Polisi watoa elimu ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi

 NA MWANDISHI WETU,  DAR ES SALAAM  


KATIKA kusherehekea siku ya wanawake duniani, Sauti ya Matumaini Foundation (SAMAF) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wameweza kutoa elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia katika shule ya sekondari ya Jamhuri jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na wanafunzi hao zaidi ya 600, Mkuu wa dawati la jinsia Mkoa wa Kipolisi Ilala, Inspekta Dk. Christina Onyango aliwataka kujiamini, kuripoti vitendo hivyo wanapofanyiwa pamoja na kujiepusha na masuala ya mitandao ya kijamii.


"Acheni kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo kwani vitendo hivyo husababisha kupata maradhi....pia acheni kuangalia picha cha ngono katika simu za wazazi wenu zinawaletea mihemko na kuwasababishia kufanya vitendo visivyofaa.


"Jiepusheni na tamaa, ridhikeni na kile ambacho wazazi wanawapatia ili msije kujiingiza katika matendo mabaya ikiwemo ya kujiuza...urithi wa kudumu na wenye faida ni elimu. Na mnapofanyiwa ukatili usikimbilie nyumbani wahi hospitali au polisi, hii itatusaidia kupata ushahidi wa awali pamoja na dawa za kuzuia maambukizi au mimba," alisema Inspekta Onyango ambaye pia ni Mratibu wa Kituo cha One Stop Center Amana.


Aidha alisema katika kituo hicho cha One Stop Center wanapokea kesi zisizopungua 20 kwa wiki huku nyingi zikiwa za ulawiti na ubakaji.




Aliongeza kuwa ndani ya miezi mitatu, kesi zipatazo 30 zinafikishwa mahakamani huku zinazopata hukumu zinafikia tatu.


"Changamoto kesi zinazokuja zinazohusisha masuala ya kifamilia hua zinakwama njiani kwasababu wanaenda kuzimalizia nyumbani jambo ambalo sio sahihi na ndio maana vitendo hivi vinaendelea kuwepo. Kwahiyo nitoe wito kwa jamii wasifumbie macho vitendo hivi, waviripoti na wasikubali kumalizana nyumbani kwani tutakaposhirikiana na wakafikishwa mahakamani itasaidia kupunguza vitendo hivi," aliongeza Inspekta Onyango.


Naye Mtendaji Mkuu wa SAMAF, Penina Malundo alisema Taasisi hiyo ilianzishwa  mwaka 2021 na kuanza rasmi kutoa huduma za kijamii, Juni 2022,lengo ikiwa kurudisha tabasamu kwa watoto wanaoishi katika Mazingira magumu ,  Walemavu kwa kuwapatia misaada mbalimbali na pia kutoa elimu ya masuala ya kujitambua kwa vijana, Ukatili wa Kijinsi na masuala ya Afya ya uzazi.


"Leo tumekusanyika hapa kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani ambapo ufanyika Machi 8 Kila Mwaka,katika kuadhimisha siku hii SAMAF imeamua kuja kuadhimisha na Wanafunzi wa Shule ya sekondari Jamhuri kwa kuja kutoa elimu ya masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya ukatili wa Kijinsia na Hedhi salama kwa watoto wa kike.


"Lengo la Samaf kuadhimisha siku hii katika shule hii ni kutoa fursa kwa wanafunzi kupatiwa elimu kwa kina kutoka kwa wataalam wetu wa masuala ya Jinsia,Afya ya uzazi  ili kuchukua hatua za kujilinda," alisema Malundo.


Alifafanua kuwa suala la Vitendo vya Ukatili wa Kijinsi  vimekuwa tishio kubwa nchini  na  kufifisha ndoto za vijana wengi hususani wanaokuwa shuleni na kuwafanya wanakatisha masomo yao.


"Wengi wao wanakatisha masomo kutokana na aibu wanayoipata baada ya kufanyiwa vitendo hivyo, wengine kupata majeraha mbalimbali ya kimwili na kifikra ambayo wanaona hawana nafasi tena ya kurudi shuleni. Sasa ni wakati wa Jamii kusimamia pamoja kuhakikisha tunazidi kupaza sauti zetu hadi vitendo hivi kutokomeza kabisaa," aliongeza Malundo.


Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jamhuri, Boniphace Mwalengo aliwashukuru SAMAF na jeshi la polisi kwa kutoa elimu hiyo ambapo alisema itasaidia kuleta mabadiliko kwa wanafunzi hao.


Mmoja wa wanafunzi hao, Athumani Ngoda alisema, "vitu vingi nilikuwa sivifahamu lakini nashukuru kupitia elimu hii tuliyopewa nimevielewa na nitavifanyia kazi,".





No comments:

Post a Comment

Pages