HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 09, 2023

Ujenzi Bwawa la Masaka wakamilika

Waandishi wa habari waliotembelea bwawa la Masaka wakipata maelezo ya bwawa hilo kutoka kwa Injinia Geofrey Simkonda ambaye ndiye msimamizi wa ujenzi wa bwawa hilo.
 

Na Irene Mark, Iringa

SERIKALI imekamilisha ujenzi wa bwawa la kuihifadhia maji lenye  urefu wa Mita 260 na kina cha futi 14 likiwa na uwezo wa kutunza maji lita za ujazo 439,803.

Ujenzi wa bwawa hilo lililopo kwenye Kata ya Masaka, Iringa Vijijini mkoani Iringa umesimamiwa na Bodi ya Maji Bonde la Rufiji (BRWB) ikiwa ni moja ya mkakati wake wa kutunza rasilimali maji na vyanzo vyake.

Injinia Geofrey Simkonda wa BRWB ambaye ni msimamizi wa ujenzi wa bwawa hilo, alisema lengo hasa ni kuwahamisha wananchi zaidi ya 12,000 wanaotumia maji ya mto Lukalama ambao maji yake huingia kwenye bonde la Rufiji.

“Baada ya utafiti tukaona hapa Masaka tunaweza kujenga bwawa hapa ambalo maji yake yatawasaidia wanavijiji hawa kwa umwagiliaji, mifugo na matumizi ya kijamii ili kupunguza kasi ya matumizi na upotevu mwingi wa maji kwenye mto Lukalama.

“Hii yote ni kuhakikisha tunapata maji ya kutosha kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo mto Lukalama na kupeleka Rufiji kwenye bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere kwaajili ya uzalishaji wa umeme wa uhakika na kuinua uchumi wa nchi yetu.

“...Ujenzi wa bwawa hili umefanyika kwa miezi sita kuanzia Mei,2022 hadi Novemba mwaka huohuo, maji yameanza kuingia ila hadi kujaa kwake matarajio yetu ni miaka miwili ikiwa mvua zitanyeesha za kutosha chini ya hapo uhakika wa kulijaza kwa mvua ni miaka mitatu ili kuruhusu wanavijiji sasa walitumie bwawa lao,” alisema Simkonda.

Akizungumza na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari waliotembelea bwawa hilo, Diwani wa Masaka, Methew Nganyagwa, aliishukuru serikali kwa ujenzi huo aliosema ni mkombozi wa uchumi kwa wana Masaka na Iringa vijijini.

Alisema kata ya Masaka ni muungano wa vijiji vitatu ambavyo ni Makota, Sadani na Kaning’ombe ambavyo asilimia 90 ya wakazi wake ni wakulima wanaotegemea maji ya mto Lukalama.

“Naishukuru Serikali ya Rais Mama Samia Suluhu kwa kuiwezesha Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kutujengea bwawa hili la Masaka.

“Maana yake sasa tukianza kulitumia tutafanya kilimo cha umwagiliaji ambacho tija yake ni kubwa na zaidi ni kwamba tutalima msimu wote wa mwaka kwa kubadili mazao kulingana na ushauri wa mabwana shamba wetu,” alisema Nganyagwa.

Alibainisha kwamba bwawa hilo litaongeza ajira ya uvuvi kwa wakazi wa Masaka hivyo uchumi wa eneo hilo kwa miaka mitatu ijayo utakuwa bora zaidi.

Diwani Nganyagwa alisema ataendelea kuhamasisha upandaji wa miti na utunzaji wa mazingira kwenye mto Lukalama ili kupata rasilimali maji ya kutosha kwenye mto huo unaomwaga maji yake kwenye mto Ruaha mdogo.

“Awali wananchi kwa kuwa ni lazima watumie maji, walikuwa wakiingia kwenye vyanzo vya maji vya asili, mito na vijito kisha kuharibu vyanzo hivyo vya maji vya asili kutokana na shughuli za kilimo, ufugaji na matumizi mengine,” alisema Diwani Nganyagwa.

Alisema ni vema kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa mabwawa kwa kushirikiana na wananchi ili kuokoa vyanzo vya maji huku ujenzi wake ukiwa rahisi kwani unafanywa na wataalamu wazawa.

No comments:

Post a Comment

Pages