Na Victor Masangu, Kibaha
Baadhi
ya wanafunzi wa kike wanaosoma katika shule za msingi na sekondari
katika halmashauri ya mji Kibaha bado wanakabiliwa na changamoto mbali
mbali ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia pamoja na ukosefu wa mahitaji
muhimu ikiwemo taulo za kike.
Kwa
kuliona hilo wafanyakazi wanawake wa kampuni ya SF Group ya Jijini Dar
es Salaam wameamua kutumia maadhimisho siku ya wanawake duniani kufanya
matendo ya huruma katika kata ya sofu kwa baadhi ya maeneo.
Wafanyakazi
hao wa SF group ambao wameona kuna haja ya kuitumia siku hiyo hivyo
kuungana kwa pamoja na kwenza kutoa misaada mbali mbali kwa wanafunzi wa
shule ya Koka sekondari pamoja na kituo Cha watoto yatima na wanaishi
katika mazingira magumu.
Akizungumza
kwa niaba ya wafanyakazi wenzake katika ziara hiyo Aisha Kanyika
alisema kwamba wametoa msaada wa vitu mbali mbali katika shule ya Koka
sekondari ikiwemo taulo kwa ajili ya wanafunzi wa kike ili ziweze
kuwasaidia kusoma katika mazingira rafiki.
"Mimi
pamoja na wenzangu tupo hapa kwa ajili ya kutoa msaada wa vitu mbali
mbali katika shule hii ya Koka sekondari na pia tunamshukuru Mwenyekiti
wetu wa SF mheshimiwa Koka pamoja na mkewe ambao wameweza kuhakikisha
wanafanikisha shughuli hii,"Alibainisha Aisha.
Aidha
Aisha alisema kwamba lengo lao ni kuendelea kuisaidia jamii katika
nyanja mbali mbali na kuwahasa wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii ili
waweze kutimiza malengo ambayo wamejiwekea katika siku za baadae na kuwa
ni nidhamu kwa walimu wao.
Pia
katika ziara hiyo wafanyakazi hao walitembelea kituo Cha watoto yatima
na ambao wanaishi katika mazingira magumu ambapo walitoa msaada wa
vyakula mbali mbali ikiwemo unga,mafuta ya kupikia,madaftari,maji ya
kunywa,miswaki na mahitaji mengine muhimu pamoja na fedha.
Naye
Kaimu mwalimu mkuu wa shule ya Koka Sekondari Godwin Magoha
aliwashukuru wafanyakazi hao kwa moyo wa kujitolea na kwenda kutoa
msaada wa vitu mbali mbali ambavyo vitakuwa ni msaada hasa kwa watoto wa
kike.
Kwa upande wake
Mkurugenzi ambaye pia ni mmiliki wa kituo cha Buloma Anna Kiando
amebainisha kwamba amefurahishwa sana na kitendo cha wafanyakazi hao wa
SF Group kutenga muda wao na kutoa msaada kwa watoto hao ambao kwao ni
mkombozi mkubwa kulingana na mahitaji waliyopatiwa.
Elina
Mgonja ni Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha mji naye hakusita
kuwapongeza wafanyakazi hao kwa kuonyesha uzalendo kwa watu wenye
mahitaji pamoja na kumshukuru Mbunge wa Jimbo la Kibaha mji Silvestry
Koka pamoja na mke wake kwa kusaidia makundi ya watu wenye mahitaji.
Ziara
ya wafanyakazi wanawake wa kampuni ya SF Group katika kata ya sofu
imeleta neema kubwa kwa wanafunzi wa kike katika shule ya Koka sekondari
pamoja na kituo cha watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu
cha Buloma kutoka na misaada waliyopatiwa.
No comments:
Post a Comment