Na Mwandishi Wetu
Klabu ya Simba imefanikiwa kujikusanyia pointi tatu muhimu kwa Vipers FC ya Uganda jioni ya leo kwa ushindi wa bao (1-0).
Kwa ushidi huo Simba imefikisha pointi sita zinazoisogeza hadi nafasi ya pili kwenye kundi C hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL nyuma ya Raja Casablanca wenye pointi 12 baada ya kushinda jioni ya leo dhidi ya Horoya AC ugenini.
Mchezo wa leo Simba wakihitaji ushindi pekee Ili kuendelea kujiweka sawa katika mbio za kuisaka nafasi ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa Barani Afrika.
Dakika ya 45 Clatous Chota Chama Mwamba wa Lusaka alifanya yake baada ya makosa ya safu ya ulinzi ya Vipers na kuiandikia Simba bao la uongozi lililodumu dakika 90 za mchezo.
Simba licha ya ushindi wa leo lakini hawakuwa na mchezo mzuri kama ambavyo mashabiki na wapenzi wa Soka walitaraji kuona kikosi cha Mnyama kinarejesha ufalme wake wa kutembeza boli na kushinda kwa ushawishi.
Simba wakati ikiwa na mpira mara kadhaa ilikuwa inakosa utulivu na kupoteza mipira kirahisi na wakati wakiwa bila mpira walikosa umbo la kiulizi jambo lililopelekea kuwa matatizoni nyakati ambazo Vipers walijaribu kuwahadaa.
Vipers walikosa tu ufanisi katika safu ya ushambuliaji Ili kuweza kuondoka na pointi moja ama tatu zote kwa namna ambavyo Simba walikuwa wanacheza.
Simba itahitaji kumfunga Horoya AC mchezo unaofuata katika Dimba la Benjamin Mkapa wikiendi ijayo Ili kutinga hatua ya Robo Fainali kwani watafukisha pointi 9 ambazo Vipers na Horoya hawataweza kuzifikia.
No comments:
Post a Comment