HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 03, 2023

NGO's 29 zilizotuhumiwa na Dk. Mwakyembe kusambaza ushoga kikaangoni

Na Janeth Jovin

BARAZA la Taifa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NACoNGO), limeanza kuzihoji NGO's 29 na aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe  dhidi ya tuhuma za uwepo wa shughuli za  vitendo vya ushoga (LGBTQ) nchini zilizoibuliwa hivi karibuni na waziri huyo wa zamani.



Akizungumza na waandishi wa habari  Jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa NACoNGO, Dk. Lilian Badi, amesema Kamati tendaji kwa kushirikiana na Kamati ndogo ya maadili ya baraza hilo, imeanza kumuhoji Waziri huyo wa zamani juu ya utafiti wake aliyofanya hivi karibuni uliotaja  mashirika yanayofanya shughuli hizo.

Dk. Badi amesema, Dk. Mwakyembe  atahojiwa ili kueleza kinagaubaga kuhusu utafiti wake huo uliobaini uwepo wa baadhi ya NGO's zinazohamasisha vitendo vya ushoga nchini, kinyume cha sheria na maadili.

"Tumefanya kikao cha dharura cha Kamati tendaji ili kujadili, kuchanganua hali na kuweka maazimio ya utekelezaji kuhusiana na suala hili,hata hivyo kumefanyika mawasiliano ya awali na mashirika yote yaliyohusishwa ikiwa ni maandalizi ya kuwafanya uchunguzi na mahojiano ya kina, kamati yetu inaandaa namna bora yakufanya zoezi la uchunguzi," amesema na kuongeza kuwa

"Tumeomba kukutana na kamati ya Dk. Mwakyembe ili tupate taarifa yao na pia tuwaeleze maoni yetu na Juhudi tunazozichukua kama viongozi wa sekta ya NGO's baada ya kukamilisha hayo tutaandaa taarifa yetu pamoja na kutoa tamko kwa umma kwa watanzania hususani wadau na wabia wa shughuli za NGO's nchini,"amesema.

Aidha amesema Dk. Mwakyembe atawaeleza alifanyaje tafiti, amegundua nini na  kwa nini aliamua kutoa taarifa hivyo . Hivyo anatoa maelezo yake yakikamilika NACoNGO itatoa taarifa kwa umma.

Amesema baada ya kamati hizo kumaliza kuwahoji wahusika wote  hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mashirika yatakayobainika kuhusika na vitendo hivyo.

Mwenyekiti huyo wa NACoNGO, alitaka sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali kuwa watulivu katika kipindi ambacho baraza hilo linafanyia kazi tuhuma zinazoibuliwa.

"Kama NACoNGO tunataka kuilinda jamii yetu na kubaki salama katika suala hili lililokinyume na maadili ni vyema kuungana kuwa pamoja kuliko kunyoosheana vidole,hivyo wanasekta ya NGOs tuepuke kuhukumu baadhi ya makundi ama taasisi hadi hapotutakapokuwa na taarifa kamili na kudhibitika bila mashaka kuwa watu fulani au makundi fulani wamehusika,"amesema Dk. Badi.

Hata hivyo amesema mijadala kuhusu suala hilo ingoje taarifa rasmi ya NaCoNGO kuhusu hali halisi itakayotia ndani uchunguzi kwa mashirika yote yaliyohusishwa na tuhuma hizo,na pia taarifa yao itafikishwa katika bodi ya uratibu ya NGO's kupitia Ofisi ya msajili wa NGO's Tanzania Bara

No comments:

Post a Comment

Pages