HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 29, 2023

Benki ya NMB yatia fora ulipaji kodi serikalini


Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akisikiliza Maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa Benki ya NMB, Alfred Shao wakati alipotembelea Banda la NMB wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 37 Jumuia ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaoendelea jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angella Kairuki, Mkuu wa Mkoa wa Arusha John   Mongela (watatu kulia) Pamoja na Makamu Mwenyekiti wa ALAT Bw. Sima Constatine (wanne kulia). 

 

Na Mwandishi Wetu

 

Mafanikio makubwa ya kiutendaji ambayo Benki ya NMB imeyapata miaka ya hivi karibuni na kupelekea kuchangia kwa kiasi kikubwa juhudi za ujenzi wa taifa ni matokeo ya Serikali ya Awamu ya Sita kuboresha na kuendelea kuweka mazingisha wezeshi ya biashara nchini.

Ufanisi huo umebainishwa jana jijini Arusha na maafisa waandamizi wa benki hiyo kwenye mkutano wa 37 wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT Taifa) wakati walipowasilisha inachokifanya taasisi hiyo katika maendeleo ya nchi ikiwemo kulipa kodi zenye thamani ya TZS trilioni 1.3 ndani ya kipindi cha miaka minane.

Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali, Bw Alfred Shao, aliuambia mkutano huo kuwa mchango wa serikali kwa wao kufanya vizuri katika viashiria vyote muhimu vya biashara ya benki ni mkubwa na inastahili pongezi kwa hilo.

Alipotembelea banda la benki hiyo kabla ya kufungua rasmi mkutano mkuu wa mwaka huu wa ALAT, Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango, aliambiwa na Bw Shao kuwa NMB si tu ni mlipakodi mkubwa nchini lakini pia ni kinara wa kukusanya mapato ya serikali na shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo ustawi wa jamii.

Hilo lilimfurahisha sana kiongozi huyo ambaye alisema ni vitu vya msingi kama hivyo ndiyo vinaifanya Benki ya NMB kuwa faraja ya Watanzania.

Akisisitiza umuhimu wa kuyatunza mazingira katika hotuba yake kwa ajili ya maendeleo endelevu, Dkt alipendekeza kuwa ili zishiriki kikamilifu katika ajenda hiyo kuna haja ya kuzishindanisha halmashauri zote kwenye kuyatunza na kuyalinda mazingira.

“Nadhani tufanye kama NMB walivyofanya kwenye kampeni ya kupanda miti milioni moja ambapo kwa kushirikiana na TAMISEMI wameandaa shindano la shule la upandaji miti lenye zawadi zenye thamani ya TZS 472 milioni kwa ajili ya washindi na washiriki wake,” Dr Mpango alipendekeza kwa Waziri Angela Kairuki.

Aidha, Makamu huyo wa Rais, amezitaka halmashauri zote nchini na serkiali za mitaa kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha zinazotolewa na serikali, kuongeza nguvu kwenye ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma.

Bw Shao alisema kupitia mifumo yao bora na rahisi wameweza kuisadia Serikali katika makusanyo ya mapato ambapo NMB imeweza kukusanya zaidi ya TZS trilioni 9.8 kuanzia mwaka 2018.

Akifafanua kwenye mkutano wa ALAT, alisema ufanisi huo wa kipekee uliwezeshwa na mifumo yao ya kidijitali kama vile NMB Wakala, internet banking and NMB Mkononi pamoja na mtandao mpana wa matawi 228 yaliyokuwa kwenye kila halmashauri nchi nzima hadi mwaka jana.

Afisa huyo pia alimwambia Dkt Mpango kuwa kwa mara nyingine tena NMB ndiye mfadhili mkuu wa mkutano mkuu wa ALAT ambao imeufadhili kwa TZS milioni 200 na kwa miaka saba mfululizo ikichangia zaidi ya TZS billion 1.2 kusaidia kuiandaa.

“Kama ambavyo kauli mbiu ya mkutano huu inavyosema - ‘Miundombinu Iliyoboreshwa ni Chachu ya Utoaji wa Huduma Bora katika Mamlaka za Serikali za Mitaa’ - Benki ya NMB imekuwa  mshirika mkubwa  sana kupitia halmashauri zetu katika kuboresha miundombinu ya elimu, afya, usafirishaji na mazingira,” alibainisha.

“Lengo kuu la hilo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na utoaji wa huduma bora kwa Watanzania,” alisisitiza na kusema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu benki yao imetoa kiasi cha TZS bilioni 4.9 katika kusaidia sekta za afya na elimu.

Bw Shao aliongeza kuwa tuzo za ukubwa wa kodi wanazolipa na ulipaji wake kwa hiari walizopata mwaka jana ni kielelezo cha mchango wa benki hiyo kwenye ukuaji wa uchumi nchini na maendeleo ya kiuchumi ya taifa kwa ujumla.

Aidha, alikili kuwa hilo na michango mingine ya maendeleo ya NMB ni  matokeo ya kuboreshwa kwa mazingira ya biashara yanayosaidia sekta binafsi nchini kushamili na kuiongezea serikali nguvu kuboresha maisha ya wananchi na kujenga nchi kwa ujumla.

Afisa huyo mwandamizi wa NMB alitolea mfano wa faida baada ya kodi ya TZS bilioni 432 ambayo waliipata mwaka jana na kuweza kutenga kiasi cha TZS bilioni 6.2 kwa ajili ya bajeti ya kuwajibika kwa jamii (CSR) mwaka huu ambapo ziada ya TZS 2 bilioni kwenye kiasi ambacho kingetengwa kama sera ya CSR inavyoelekeza ni kwa ajili ya kutekeleza ajenda ya uendelevu ya benki hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages