HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 29, 2023

SMZ KUWACHUKULIA HATUA KALI WAVAMIZI WA ARDHI YALIYOTENGWA

WAZIRI wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Rahma Kassim Ali amesema kumekuwa na uvamizi wa uuzaji wa maeneo ya ardhi ya akiba yaliyotengwa kwa ajili mpango wa matumizi ya Serikali katika shughuli za kimaendeleo.

Aliyasema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Paje Mkoa wa Kusini Unguja katika kikao maalumu cha utoaji elimu kuhusiana na maeneo ya ardhi ambayo Serikali imeyatenga kwa ajili ya shughuli hizo na kuonekana kuvamiwa na kuuzwa viwanja kiholela kinyume na utaratibu.

Alifahamisha kuwa miongoni mwa maeneo ya ardhi ya akiba ni ukanda wa paje ambapo imeonekana kushamiri kwa uvamizi kwa vile maeneo mengi ya ukanda huo ni ya uwekezaji hivyo mtu yoyote akitaka kuhaulisha eneo lake ikigundulika eneo hilo limo katika mpango wa Serikali basi hatohaulishiwa.

“kwa kweli inasikitisha kuona kuwa ukanda wa paje unaongoza kwa uuzaji wa maeneo ya ardhi ya akiba kitendo ambacho si cha kiungwana  hivyo naomba tuache mara moja kujishughulisha na vitendo hivyo”alisisitiza Waziri Rahma.

Alifahamisha kuwa zoezi hilo la utoaji elimu ni endelevu kwa unguja nzima kwani moja ya dhamira na malengo ya Serikali ni kuona kuwa maeneo yote yaliyotengwa kwa shughuli hizo yanatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili kuipa thamani ardhi ya Zanzibar.

“sisi wenyewe tunatakiwa kuithamini ardhi yetu na sio kuuza kiholela kwa faida ya vizazi vya baadae”alisema Waziri Rahma.

Aidha Mhe. Rahma alifahamisha kuwa kamisheni ya ardhi imekuwa ikipokea maombi mengi ya uhaulishaji wa maeneo ambapo ndio miongoni mwa jukumu la kamisheni ya ardhi kisheria na kubaini kuwa baaadhi ya maeneo yaliyoombewa uhaulishaji ni ya ardhi ya akiba hivyo ni vyema wananchi wakafatilia maeneo yao kabla ya kufanya uhaulishaji ili kuweza kuepusha migogoro ya ardhi inayoweza kuepukika.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi amesema kamisheni kushirikiana na Wizara ya ardhi imeandaa mpango maalum ikiwemo utoaji wa elimu katika vijiji vyote vyenye kuanisha ardhi ya akiba na kuyadhibiti na kuanzia sasa yoyote atakaekwenda kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria hatua kali ziatchukuliwa dhidi yake.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmin Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja Rajab Yussuf Mkasaba ameiomba wizara ya ardhi kuhakikisha elimu inaendelea katika mikoa yote ya unguja  hasa katika vijiji vyenye maeneo ya uwekezaji pamoja na kuandaa mikakati madhubuti wa kuyadhibiti maeneo hayoyasivamiwe kiholela na kufanyiwa hujuma.

Nae Sheha wa Shehia ya Paje Mohamed Rajab Makame aliahidi kulisimamia ipasavyo suala hilo pamoja na kuiomba wizara ya ardhi kuharakisha utoaji wa hati za maeneo ya ambayo tayari yalishafanyiwa utambuzi kwa muda mrefu ili wananchi waweze kunufaika na hati hizo kwani wamekuwa wakipata usumbufu wanapokwenda kuchukua mikopo.

Nao wanakijiji wa Shehia ya Paje wameipongeza wizara kwa kuwapatia elimu hiyo na wmaeahidi kuifanyia kazi sambamba na kuomba kuwekewa alama maalumu zitakazoweza kuonesha maeneo yote yaliyo katika mpango maalum wa Serikali.

No comments:

Post a Comment

Pages