HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 30, 2023

Ujenzi Hospital Mpya Handeni wafikia asilimia 98

 Na Mashaka Mhando, Handeni


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tanga, kimeridhishwa na ujenzi wa hospital mpya iliyojengwa katika mji wa Mkata wilayani Handeni kwa gharama ya kiasi cha shilingi bilioni 5.8.



Akizungumza baada ya kuitembelea hospital hiyo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman Abdalah alisema chama kimeridhishwa na ujenzi huo na kinaunga na halmashauri kumpongeza Rais Dkt Samia kwa kazi kubwa anayoifanya katika sekta ya afya.


Alisema Rais katika sekta ya afya katika mkoa wa Tanga ameleta fedha nyingi ambazo zimeweza kujenga hospital, vituo vya afya na zahanati pamoja na kutoa fedha kukarabati hospital zilizokuwa kongwe mkoani hapa.


"Kwa miaka miwili ya uongozi wake Rais Dkt Samia sisi watu wa mkoa wa Tanga ametupatia kiasi cha sh. 83,542,389,222. Tuna kila sababu ya kumzungumzia vizuri Rais wetu kwa upendo huu," alisema na kuaahidi kwamba mkoa huo utaongoza kwa kumpa kura nyingi mwaka 2025.


Akitoa taarifa ya ujenzi ulipofikia Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Handeni Dkt Kanansia Shoo alisema serikali iliwapa fedha kiasi cha sh. 2,884,000,000 na kuanza kutekeleza mradi huo ambao ulinza mwaka 2013 katika hatua ya awali.


Alisema fedha nyingi za kukamilisha ujenzi huo zililetwa mwaka 2022 zikatumika kujenga jengo la maabara, wagonjwa wa nje, bohari ya dawa, wodi ya wanawake na wanaume, jengo la upasuaji, la dharura na wodi ya watoto.


Pia katika fedha hizo kiasi cha shilingi milioni 300 zilinunulia vifaa tiba, samani na kuweka mifumo ya teklonojia ya habari na mawasiliano (Tehama).


Dkt Shoo alisema kwa upande wa wadau wa Islamic Help wameweza kutoa kiasi cha sh. 2,947,316,405.51 fedha ambazo zimetumika kujenga jengo la mama na mtoto, jengo la mionzi na jengo la kufulia.


Kazi nyingine zilizofanyika kupitia fedha hizo ni kujenga jengo la kichomea taka, utawala, kuhifadhia maiti, kazi za nje, ujenzi wa uzio na walk ways na vifaa vya hospital na samani.


"Kwa ujumla jengo limekamilika kwa kiwango cha asilimia 98 na serikali tayari imeleta wataalamu wa kada mbalimbali wapatao 30 ingawa mahitaji kwa hospital hiyo ni watumishi 200 hadi 312," alisema Dkt Shoo.


Mganga huyo alisema matarajio ya hospital hiyo ni kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa wanaokadiriwa kufikia watu 409,158 pamoja na wananchi wengine wa maeneo jirani.


"Ujenzi wa hospital hii ni matokeo ya juhudi za serikali ya awamu ya sita, katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi. Tunatoa shukrani za dhati kwa serikali ya awamu ya sita ikiongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan," alisema Dkt Shoo.

No comments:

Post a Comment

Pages