Kutoka kulia Wanariadha wa kimataifa wa Tanzania wanaopeperusha vema bendera ya Tanzania kimataifa, Alphonce Simbu na Gabriel Gray, walipoalikwa kupongezwa bungeni jijini Dodoma, hivi karibuni.
Na Mwandishi Wetu
KESI ya madai waliyofungua Wanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Felix Simbu, Gabriel Gerald Geay na Failuna Matanga dhidi ya Kampuni ya Multi Choice Tanzania imefikia hatua ya utekelezaji.
Katika kesi hiyo, Simbu na wenzake waliiomba Mahakama iwaamuru wadaiwa Multichoice Tanzania kuwalipa Sh. Bilioni moja kila mmoja, kwa kile walichodai kuwa matumizi ya kibiashara ya picha zao bila ridhaa zao mnamo mwaka 2021, wakati wakielekea Tokyo nchini Japan kwenye michezo ya Olympiki.
Simbu na wenzake, walipata ushindi katika kesi hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha, ambayo iliamuru walipwe Sh. Milioni 150 kila mmoja badala ya Sh. Bilioni moja walizoomba kwa kila mmoja.
Kwa taarifa ambazo Habari Mseto inazo, kesi hiyo imefikia hatua ya utekelezaji na Mahakama ya Wilaya ya Arusha imeishatoa amri kwa Benki ya NMB kuwalipa kina Simbu kwa kutoa fedha kutoka kwenye akaunti za Multi Choice zilizopo NMB Bank. (Nakala ya amri hiyo Habari Mseto inayo).
Hata hivyo, chanzo chetu kinaeleza kwamba, pamoja na kwamba hakuna rufaa ambayo Multi Choice wamekata mpaka sasa, lakini inastaajabisha kuona kuwa amri hiyo ya mahakama haitekelezwi. Zaidi inasemekana Multi Choice wamefungua kesi mbili tofauti, wakiomba zuio la utekelezaji wa hukumu hiyo bila kuwa na rufaa.
Kesi ya kwanza ni namba 04/2023 ambayo iko Mahakama Kuu kitengo cha biashara mjini Arusha na kesi nyingine namba 78/2023 ambayo iko Mahakama Kuu kitengo cha Biashara Dar es Salaam.
Habari Mseto ilimtafuta Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wakili Jackson Ndaweka, ambaye alisita kuongelea kwa kuwa kesi zinaendelea mahakamani na yeye si wakili wa wadai, lakini alieleza kuwa hata yeye amesikia kwamba kuna kesi mbili zote za zuio la utekelezaji, moja iko Arusha na nyingine imefunguliwa jijini Dar Salaam zote zikihusu jambo hilo moja. Amesema kwa kuwa yeye si wakili wa wadai hawezi kujua kiundani kwanini imekuwa hivyo.
Wachezaji husika walipotafutwa, wamesema wanachoona wao ni ucheleweshaji tu wa haki zao. Lakini wanayo imani kubwa na mahakama na wanaamini haki zao zinaweza kucheleweshwa lakini hazitapotea.
Kesi ya zuio iliyopo Arusha imepangwa kusikilizwa tarehe 05/06/2023 wakati ile ya Dar imepangwa kusikilizwa tarehe 08/06/2023.
No comments:
Post a Comment