HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 27, 2023

Raia wa Marekani ahukumiwa jela miaka 20

 Na Mwandishi Wetu


MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imemuhukumu  Lione Lionel Rayford raia wa Marekani kifungo cha miaka 20 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 2.188.


Hukumu hiyo imetolewa juzi kufuatia shauri la uhujumu uchumi namba 17 la mwaka 2021 lililokuwa mbele ya Jaji Isaya kumalizika pasipo shaka kwamba, mshtakiwa alijihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya.


Mtiwa hatiani alikamatwa  na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Julai 5, 2018 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  akiwa ameficha dawa hizo katika moja ya mabegi aliyokuwa nayo.


Upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliwakilishwa na Clara Charwe, Erick Shija na Moses Mafuru Mawakili wa Serikali na jumla ya Mashahidi 15 wa upande wa mashtaka walitoa ushahidi wao katika kuthibitisha kosa la mtuhumiwa huyo kusafirisha dawa hizo za kulevya.


Kwa upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili Omari Kilwanda ambapo ulileta shahidi mmoja na mshtakiwa alijitetea mwenyewe.


Wakili upande wa Jamhuri, Mafuru wakati akiwasilisha hoja za upande wa mashtaka za kuomba adhabu kali dhidi ya mtuhumiwa alidai kiasi cha dawa kilikuwa ni kikubwa hivyo kilikuwa kinakwenda kuharibu na kuathiri sehemu kubwa ya jamii.


Pia alidai kuwa madhara ya dawa za kulevya kama yalivyo elezwa katika taarifa ya Mkemia yanasababisha ulevi usio ponyeka, yana sababisha kuharibikiwa na akili na ni dawa ambazo zipo kwenye kundi la sumu, hivyo athari zake ni mbaya na zenye madhara makubwa kwenye afya ya binadamu.


Nao upande wa mtuhumiwa ulitaka mahakaa impunguzie adhabu  anafamilia kwa maana ya mke na watoto wanaomtegemea hivyo ni busara kupewa adhabu ndogo ili awe na nafasi ya kuendelea kuhudumia familia inayomtegemea.


Akitoa hukumu mara baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Jaji Isaya alisema adhabu ya Mahakama imezingatia maoni ya upande wa mashtaka kuhusu athari za dawa za kilevya kiafya, kijamii, kiuchumi na kimataifa.


Pia imezingatia pia kiasi kikubwa cha dawa ambacho mshtakiwa amekutwa nacho na kwamba madhara yake ni makubwa kwa sehemu kubwa kwa jamii.


"Mahakama imezingatia pia mtuhumiwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na anaumri mkubwa. Katika kuzingatia maoni ya pande zote mbili Mahakama inatoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 gerezani. Pamoja na adhabu hii Mahakama inatoa amri kuwa kielelezo P4 na P5 viharibiwe kwa mujibu wa sheria ya madawa.


"Hati ya kusafiria (passport) zikabidhiwe kwa mamlaka ya uhamiaji kwa taratibu zao, vitu vya mtuhumiwa ikiwemo nguo za kimasai, pamoja na pesa ambazo upande wa mashtaka hawakuleta ushahidi kuonyesha kama zilihusika kutenda uhalifu, vyote virudishwe kwa mtuhumiwa," alisema Jaji Isaya.



No comments:

Post a Comment

Pages